RIYAD, SAUDI ARABIA

SAUDI ARABIA imeidhinisha chanjo mbili za corona za China na kutangaza kuwa,Waislamu wote waliochanja chanjo mbili za China yaani Sinopharm na Sinovac wanaweza kwenda nchini humo kwa ajili ya ibada ya Hija.

Saudi Arabia ilitangaza kuwa, imeidhinisha chanjo nyengine mbili za Sinovac na Sinopharm kutoka China.

Ofisa wa ngazi ya juu wa Wizara ya Masuala ya Hija na Umrah wa Saudi Arabia alisema kuwa, hatimaye shaka kuhusu uwezekano wa raia wa Bangladesh ambao wamepata chanjo ya corona aina ya Sinopharm kwenda Makka kufanya ibada ya Umrah imeondoka baada ya Riyadh kuidhinisha chanjo hizo mbili za China.

Awali Saudi Arabia iliidhinisha kutumiwa chanjo nne tu za corona yaani Oxford Astra-Zeneca, Pfizer Bion Tech, Johnson & Johnson na Moderna.

Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, wale waliochanja chanjo za corona za Sinocav na Sinopharm wanaweza kuelekea nchini humo kwa sharti kwamba, wawe wamepata chanjo ya nyongeza iliyopasishwa nchini humo.

Kabla ya hapo,Saudia ilikuwa imetangaza, watu wote waliochanjwa dozi moja ya corona aina ya Sinopharm au Sinovac wakitaka kuingia nchini humo ni lazima wachanje dozi ya pili kwa kuchagua moja ya chanjo nne ilizozipasisha.

Aidha watu hao wanalazimika kupima kipimo cha corona cha PCR kwa uchache masaa 72 kabla ya kuingia Saudia.