NA ASIA MWALIM

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, DK. Khalid Mohammed Salum, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kuwawezesha vijana kukua kiuchumi hasa katika kuzitumia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu.

Aliyasema hayo alipokua akifungua kongamano la vijana, kuadhimisha siku ya vijana lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil, Kikwajuni Zanzibar hivi karibuni.

Alisema ipo haja kwa vijana kutumia teknelojia za kisasa kukuza kazi zao za ujasiriamali na shughuli nyengine ikiwemo za bahari ili kujikwamua na hali ngumu ya kimaisha sambamba na kukuza uchumi wa nchi.

Aidha alisema ni vyema kuwa na maadalizi yao wenyewe kwa kubadilisha fikra zao na kuweka uelewa mpana wa kutumia fursa zinazopatikana kuupitia uchumi wa buluu.

Waziri huyo alisema vijana wana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar  kutokana na kufanya shughuli mbalimbali za kuingiza mapato hivyo wanapaswa kuongeza nguvu kazi ya matumizi ya ICT kwenye uchumi wa buluu ili kuleta maendeleo yao na  taifa kiujumla.

Aidha alisema njia ya teknelojia itakwenda kurahisisha kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa wakati jambo ambalo litasaidia kuwahamasisha vijana wengi  kuacha vitendo visivyo faa.

Dk. Khalid alisema katika kukuza shughuli za maendeleo na uchumi wa buluu nchini Serikali imepanga mikakati ya kuitumia bahari ipasavyo kwa kuhakikisha wavuvi wanafika kina kirefu cha maji ili kupata samaki wengi zaidi.

Aidha alieleza kuwa hali hiyo itawezesha maendeleo ya viwanda kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kuchakata samaki ili kupata samaki walio bora sambamba na kutoa ajira kwa vijana wa Zanzibar.

Alisema serikali ya awamu ya nane imelenga kuwekeza katika suala la uchumi wa buluu kwani ni sekta yenye uwanja mpana kwa kuwapatia fursa vijana, hivyo aliwataka vijana kuchangamkia fursa kwa kutumia teknelojia kwa lengo la kukuza uchumi huo.

Alisema maeneo ya bahari hutoa fursa nyingi kwa vijana kulingana na matumizi mbalimbali ikwemo shughuli za usafirishaji, utalii na uvuvi, hivyo elimu zaidi inahitajika ili kukuza maendeleo ya Zanzibar.