Zimo za mizigo, yakusanya trilioni 1.84 /-

NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema itanunua ndege nyengine tano ikiwemo ya mizigo itakayosafirisha bidhaa za kilimo na uvuvi kwenda nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema hayo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari.

Aidha, alisema Tanzania imekusanya shilingi trilioni 1.84 kwa mwezi Julai ambayo ni ukusanyaji wa juu.

Msigwa alikuwa akizungumzia miradi mbali mbali ya serikali inayoendelea ikiwa ni taarifa ya robo ya mwisho wa mwaka wa fedha kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Alisema serikali kupitia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) imesaini mkataba na watengezaji wa ndege hizo, ambazo hazihusiani na zile 11 za awali zilizonunuliwa na serikali, ambapo hadi sasa tisa tayari  zimewasili nchini.

Alisema kati ya ndege hizo, moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na nyengine ya mizigo.

Alisema Tanzania inafanya vizuri katika uzalishaji wa matunda, mboga na minofu ya samaki na bidhaa nyengine ili kuzipeleka nje ya nchi.

Alisema ndege nyengine mbili ni za masafa ya kati Air Bus A220-300 zenye uwezo wa kuchukua abiria kati ya 160-170 na moja ya masafa mafupi- Bombadier Dash 8-Q400, yenye uwezo wa kubeba abiria 76.

Alisema ndege hizo zitaimarisha uchumi wa Tanzania na kukuza sekta ya utalii.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan, amelekeza kwamba hataki ukusanyaji wa kodi wa kutumia mabavu badala yake kodi zikusanywe kwa weledi.

Alisema katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2021, serikali imekusanya jumla ya shilingi trilioni 4.41, sawa na wastaani wa shilingi trilioni 1.51 kwa mwezi.

Alieleza kuwa ulipaji kodi sio adhabu bali ni uzalendo, hivyo aliwaomba Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari.

Alisema kwa halmashauri zinazokusanya mapato yasiyozidi shilingi bilioni tano kwa mwaka, zinatakiwa zielekeze asilimia 60 ya mapato katika miradi ya maendeleo badala ya fedha kubakia mifukoni na kugawa posho.

Alisema kwa mwaka 2021 katika utekelezaji wa agizo hilo, mapato ya halmashauri yameimarika kwa asilimia 93.

Kuhusu toza ya miamala ya simu, alisema lengo fedha zinazokusanywa zitumike katika ujenzi wa miundombinu ya barabara vijijini, miradi ya maji na vituo vya afya kwa sababu viliopo sasa havitoshi.

Hata hivyo, alisema Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia na Habari kukaa ili kupitia upya tozo hizo ili kuleta unafuu kwa wananchi.