NA ABDI SULEIMAN
WAZIRI wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, amesema wizara itahakikisha sekta ya michezo inakuwa na kuitangaza Zanzibar pamoja na kuongeza pato la taifa.
Tabia aliyaeleza hayo katika ukumbi wa Green Folage Mgogoni Wilaya ya Chake Chake, katika hafla ya kuwapongeza mabingwa wa mashindano ya UMISSETA 2021 kanda ya Pemba kwa mpira wa miguu.
Waziri huyo alisema wakati umefika kwa Zanzibar, kuirejesha hadhi yake ya kujitangaza kimataifa kupitia michezo kama ilivyokuwa zamani.
Alisema wachezaji wengi walitoka Zanzibar na wameweza kuitangaza vizuri nchini, sasa tutahakikisha hadhi ya Zanzibar inarudi katika michezo.
Aidha alifahamisha kwamba, katika kuimarisha michezo hiyo pia wizara itahakikisha inaimarisha na kurudisha michezo mbali mbali ya wanawake kama ilivyo kwa upande wa wanaume.
Aliwataka wafanyabiashara na wazalendo kujitokeza kusaidia katika sekta ya michezo, kwani sekta hiyo inaitaka wizara kuinua vipaji, wachezaji wanawake kuwanyanyua katika sekta hiyo, pamoja na kuendeleza michezo.
Alisema changamoto kubwa ni vifaa vya michezo na muda wa kukaa kambini, pamoja na bajeti nitahakikisha hilo litawezekana kwa ikiwa wafanyabiashara nao watatuunga mkono.
Naye katibu Mkuu wa Wizara hiyo Fatma Hamad Rajab, alisema Wizara ya Habari ndio wasimamizi wakubwa wa michezo nchini, licha ya Wizara ya Elimu kuwa mlezi wa vijana wakati wanapokuwa maskulini.
Nae mdau wa michezo nchini, Mohammeda Raza alisema ataendelea kushirikiana na serekali katika kusaidia sekta michezo, na kuwataka wanafunzi hao kudumisha nidhamu ya michezo na kuzingatia masomo.