NA MADINA ISSA

HATIMAYE wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imefikia uamuzi wa kurasimisha biashara ya usafiri wa bajaji na pikipiki maarufu kama bodaboda, ambapo vyombo hivyo vitatumika kwa ajili ya usafiri wa umma.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, waziri wa wizara hiyo, Rahma Kassim Ali huko ofisini kwake Kisauni, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya vijana wengi Zanzibar kujishughulisha na biashara ya kusafirisha wananchi kwa kutumia pikipiki na bajaji ikiwa ni sehemu ya ajira inayowapatia kipato.

Waziri huyo alisema kurasimishwa kwa usafiri wa bodaboda na bajaji kunatokana na uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 48 (4) cha sheria ya usafiri barabarani namba 7 ya mwaka 2003, kuanzia leo itakuwa rasmi kwa wananchi kutumia usafiri huo.

Alifahamisha kuwa vijana waliojiajiri kupitia usafiri wa bodaboda na bajaji ni miongoni mwa ajira 300,000 alizoahidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Hata hivyo, waziri Rahma alisema pamoja na kurasimishwa kwa usafiri wa bodaboda, bajaji bado biashara hiyo haijawekewa utaratibu maalum kama zilivyo biashara nyengine jambo ambalo litasababisha changamoto katika kudhibiti vitendo vinavyokwenda kinyume na utaratibu.

Alisema wizara hiyo kupitia Mamlaka ya Usafiri na Usalama barabarani Zanzibar itatoa utaratibu maalum wa upatikanaji wa leseni za biashara kwa bodaboda na bajaji.

Waziri huyo aliwaomba wananchi wanaotaka kuingia katika biashara hiyo kufika katika Ofisi za Mamlaka kwa ajili ya kupatiwa utaratibu ikiwemo kupatiwa namba maalum za vyombo vya biashara.

Waziri huyo aliwataka wananchi wanaotarajia kufanya biashara hiyo kuhakikisha wanafuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni na waache kufanya mambo ambayo yanaweza kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Haji Ali Zubeir, akizungumza kwenye hafla hiyo alisema, kuwa huduma hiyo itatofautika na vyombo vinavyosafirisha watu wa kawaida ambapo vyombo hivyo vitakuwa na usajili maalum unaoanzia na namba ya usajili (plate number), ambapo itakuwa na mji mwekundu na maandishi ya manjano.

Aidha alisema kuwa mtoa huduma za usafiri wa bodaboda atakuwa na fomu maalum inayomtambulisha kuwa ni mtoa huduma ya usafiri wa bodaboda na anatoka wilaya gani na zitakuwa na namba maalum zitakazowatambulisha.

Alisema watoa huduma za bodaboda na bajaji watawekewa vituo maalum ambavyo vitatambulika kama ilivyokuwa vya daladala ambapo vitatangazwa rasmi.

Kuhusu madaraja ya leseni, Mkurugenzi Haji, alisema mtoa huduma ya usafiri wa bodaboda anatakiwa awe na leseni isiyopungua miaka miwili tokea kuipata na itakuwa ni daraja la ‘A’.

Sambamba na hayo, alifahamisha kuwa Mamlaka hadi sasa wamekuwa na idadi ya vyombo vya maringi mawili 13,000 vilivyosajiliwa ikiwemo vya bajaji na bodaboda.

Nao wafanyabiashara hao, wamesema kuwepo rasmi usafiri huo wataweza kuondokana na changamoto zilizokuwa zikiwakabili pamoja na kuahidi kuendelea kufuata miongozo iliyowekwa na wizara ili biashara yao iweze kwenda vizuri.

Mmoja wa madereva wa bodaboda wa Uwanja wa Ndege, Yasir Nasour, alisema kuwa hana budi kumshukuru Rais wa Zanzibar kwa kuwajali vijana wake na kuamua kipindi cha uongozi wake kuirasimisha biashara hiyo kwani vijana wamekuwa wakijiajiri na kuweza kujikimu kimaisha.