NA MADINA ISSA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inathamini michango inayotolewa na Chuo cha Kimataifa cha Bare Foot College International kilichopo nchini India katika kukiendeleza kituo kilichopo Kinyasini Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, aliyasema hayo alipokutana na ujumbe kutoka chuo hicho ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Rodrigo Paris huko ofisini kwake Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi ‘B’.

Alisema tangu kuanzishwa kwa kituo cha Bare Foot kilichopo Zanzibar kimeleta mafanikio makubwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi ambapo wamekuwa wakijikomboa kimaisha ambapo wamekuwa wakifanya shughuli zao mbalimbali.

Alisema serikali itaendeleza ushirikiano uliyopo na chuo hicho ili kupiga hatua zaidi ya kimaendeleo kwani hivi sasa wanawake zaidi ya 190 wameweza kujiajiri baada ya kumaliza mafunzo katika kituo cha bare foot Kilichopo Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, Waziri Soraga alifahamisha kuwa katika kuimarisha kituo hicho pia walisaini mkataba mpya wa uendeshaji wa kituo kilichopo Zanzibar.

Naye, Mkurugenzi wa chuo cha kimataifa kilichopo nchini India, Rodrigo Paris, alisema chuo chao kimefurahiswa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukiimarisha kituo hicho.

Aidha aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati ili kuona lengo la kituo linafanikiwa na kuweza kuwasaidia wanawake nchini kujikomboa katika umasikini.

Kituo cha Bare Foot Zanzibar kinatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki wa kisasa, ushoni wa nguo tofauti pamoja na masuala ya ufundi wa umeme wa jua kwa akinamama kwa Unguja na Pemba.