PARIS, Ufaransa
KLABU ya Liverpool imekubali dau la pauni milioni 9.5 kutoka Lyon kwa ajili ya kumuuza kiungo mshambuliaji wa Uswisi, Xherdan Shaqiri, baada ya kushindwa kukubaliana mwezi Januari.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 tayari ameshafanyiwa vipimo vya afya.
Shaqiri ameshakubaliana maslahi binafsi na Lyon na taarifa zinasema atasaini mkataba wa miaka minne mpaka mwaka 2025.
“Olympique Lyonnais inafurahi hatimaye imefikia makubaliano na Liverpool juu ya uhamisho wa kiungo wa kimataifa wa Uswisi, Xherdan Shaqiri”, ilisema, taarifa kwenye tovuti ya Lyon.
Shaqiri aliweka wazi nia yake ya kuondoka Liverpool msimu huu wa joto kutafuta nafasi ya kucheza. Anaondoka akiwa amecheza mechi 63 kwenye klabu hiyo tangu ajiunge akitokea Stoke mnamo 2018, na kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup, Klabu Bingwa ya Dunia na Ligi Kuu ya England.(Goal).