NA ASIA MWALIM

MWENYEKITI wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Khadija Shamte Mzee, amesema tume hiyo inakusudia kuanzisha chombo maalumu cha kuwalinda wahasibu wanaofanya ukaguzi wa matumizi ya fedha za serikali.

Aliyasema hayo alipokua akizungumza na wakaguzi wa ndani (CAG), kwenye mjadala kuhusu sheria namba 11 ya mwaka 2003, huko Maisara mjini Zanzibar.

Alisema chombo hicho kinakusudiwa kuweka utaratibu wa kuondoa vikwazo wanavyovipata wakati wanapotekeleza majukumu ya ukaguzi wa fedha katika taasisi mbalimbali za umma sambamba na kuwajengea uwezo wa kiutendaji.

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa si jambo jema kuona wahasibu wanaopata nafasi hizo wanatoka nje ya Zanzibar wakati watu wenye sifa hizo wapo nchini.

Alifahamisha kuwa lengo la Tume hiyo ni kuona wahasibu waliopo nchini wanakuwa na sifa na uwezo mzuri wa kutumikia nafasi hizo kwa ueledi zaidi.

Mwenyekiti huyo alisema Tume inatamani kuona wahasibu na wakaguzi wa ndani wanaziba na kutumikia nafasi hiyo isiweze kutumiwa na CPA kutoka nje ya Zanzibar.

“Mimi siamini kama hapa Zanzibar hakuna hizo sifa hata CAG anaamua kuchukua wakaguzi kutoka upande wa Tanzania bara, wakati wenye uwezo wapo”, alisema.

Aidha alisema katika kuhakikisha wanapata sheria yenye kiwango kizuri wamepanga kuangalia sheria za nchi mbalimbali kulingana na mujibu wa uzoefu wao sambamba na kutizama maeneo mazuri kiutendaji.

Aliwataka washiriki hao kutoa maoni ili kuifanya sheria hiyo iwe na usawa kwa pande zote na kupata sheria bora zaidi kwa kuondoa makosa yaliyojitokeza kulingana na wakati.

Hata hivyo aliwataka wahasibu na wanasheria kuondoa hofu kwa mswaada huo ambao umekusudia kupata sheria itakayodumu kipindi kirefu bila ya kuchezewa.

Kwa upande wake, Mwanasheria kutoka Tume ya kurekebisha sheria Said Nassor Said alisema Ofisi hiyo imeanzishwa kwa umuhimu wa kutambua misingi ya utawala bora katika kulinda na kuhifadhi mali za serikali.

Alisema wakaguzi ni watu wenye kutoa muongozo kwa kutizama maeneo yenye kasoro ili kutoa maelekezo ya kiutendaji.

Nao wakaguzi wa ndani wameshauri Tume ya kurekebisha sheria kuweka sheria itakayoondoa mivutano baina ya wakuu wa taasisi na wakaguzi ili kulazimika kutoa mashirikiano wakati wa kazi hizo.

Walisema kumekuwa na mivutano kwa baadhi ya wakuu wa taasisi kukataa kukaguliwa kutokana na dhana ya kuharibiwa kazi jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

Aidha walisema muundo wa sheria uliopo ni tegemezi hivyo wameomba kuwekewa bajeti itakayowapa uwezo wa kujitegemea kifedha katika shughuli zao.