NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

KLABU za ligi kuu Tanzania Bara Simba SC na Azam FC, jana zimepeleka wachezaji wao Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupata chanjo ya Covid- 19 .

Klabu ya Yanga wao walikwenda kupata chanjo kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.

Akizungumza na Zanzibar Leo jana, Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam FC, Zakaria Thabit, alisema katika kuunga mkono harakati za serika za kupambana na maambukizi ya Uviko- 19 jana walikwenda kupata chanjo hospitali ya Muhimbili.

Alisema wao kama taasisi ni muhimu kuwalinda watu wanaofanya nao kazi ili na wao wazilinde familia zao.

Zakaria alisema Azam ni timu ambayo itasafiri sana msimu ujao kutokana na ushiriki wake kimataifa, hivyo watakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi, hiyo wameamua kuchukua tahadhari ya kujilinda wakati wote.

Kwa upande wa Simba kupitia ukurasa wao wa ‘Facebook’ wameweka picha zikiwaonyesha baadhi ya viongozi na wachezaji na wafanyakazi wake wakichanja chanjo ya Uviko-19 (Covid-19) hospitali ya Muhimbili.