NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM 

KLABU ya Simba ya jijini imezindua rasmi App itakayokuwa na taarifa zinazohusu klabu hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari jana  jijini Dar es Salaam, Msemaji wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga, amesema wamefikia uamuzi huo wa kuwa na App ya Simba kwa ajili ya kusogeza taarifa mbali mbali za klabu hiyo kutokana na janga la Covid 19.

Alisema kupitia App hiyo wanatarajia kuwafikia  mashabiki wa klabu hiyo ambapo kila mwana Simba atatakiwa kulipa shilingi 2000 tu ili kupakua App hiyo .

Alisema zaidi Simba imeamua kuzindua jukwaa hilo la mtandaoni ikiwa ni mapinduzi makubwa ya ambapo kwa sasa dunia iko kwenye zama za taarifa na katika zama zenye taarifa Simba inakuwa klabu ya kwanza Tanzania kwenda kwenye dunia ya kidigitali.

“Simba App ni jukwaa la kidigitali ambalo wana Simba watakuwa wakipata taarifa sahihi na wakati unaofaa lakini sio tu kupata taarifa tu tutakwenda kuingiza fedha kupitia fedha ambayo itatokana na wana Simba kujiunga kwa kujisajili,” alisema Kamwaga.

Kwa upande wake Mtaalam aliyetengeneza Simba App, Given Edward kutoka My Elimu, alieleza kwamba kabla ya kuzinduliwa kwa App hiyo walifanya utafiti na kujiridhisha kuwa ni wakati sahihi kuwa na jukwaa hilo kutokana na ukubwa wa Simba.

“Simba imekuja na App  kwa sababu ya ukubwa wake lakini pia ina mashabiki mamilioni kwa mamilioni zaidi ya wale 60,000 wanaoingia uwanjani hivyo kupitia jukwaa hili tutaweza kuwafikia kwa haraka na wao kutoa maoni yao,” alieleza Given.

Sambamba na hayo, aliongeza kuwa App hiyo itasaidia kuondoa habari ya uongo na kuongeza fursa za wanachama au mashabiki wa mabingwa hao wa Tanzania bara kujuana na utapata taarifa zote muhimu za klabu hiyo.