NA KHAMISUU ABDALLAH
JESHI la Polisi mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi na dola bandia za Marekani noti 301.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Mwembemadema, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Awadh Juma Haji, alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo mbali mbali ya mji wa Zanzibar.
Alisema tukio la kwanza liliwahusisha watuhumiwa wawili waliopatikana na dawa za kulevya aina ya mirungi mafurushi 45 yenye uzito wa kilogramu 81.5 iliyokuwa imehifadhiwa ndani ya nyumba katika maeneo ya Mwembeshauri Agosti 18, mwaka huu.
Aidha aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Othman Hassan (47), mkaazi wa Mwembeshauri na Juma Rashid Bakar (36) ambae ni dereva taxi mkaazi wa Mtoni wilaya ya Magharibi ‘A’, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Kamanda Awadh alisema Agosti 14, majira ya saa 4:00 asubuhi katika mtaa wa Makadara, polisi waliwakamata watuhumiwa wanne wakiwa na bangi kilo 3.4 na chupa 14 za pombe ya kienyeji aina ya gongo zenye ujazo wa lita 1.5 kila moja.
Aliwataja watuhumiwa kuwa ni Zaid Ali Khamis (22), Suleiman Juma Makame (28) wakaazi wa Makadara, Kombo Omar Mussa (49) mkaazi wa Shaurimoyo na Mohammed Mohammed Juma (18), mkaazi wa Amani.
ACP Awadhi alieleza kuwa tukio jengine liliwahusisha Omar Ali Nassor (35) na Khadija Ali Simai (38) wote wakiwa wakaazi wa Kiembesamaki waliokamatwa Agosti 12 mwaka huu majira ya saa 5:20 asubuhi maeneo ya Kiembesamaki Uwanja wa ndege wakiwa na noti bandia za dolla za kimarekani noti 301.
“Watuhumiwa hawa walikutwa na dola hizo zenye thamani ya dolla 100 kila moja, sawa na dolla 30,100 zikiwa na thamani ya shilingi 69,771,800 kwa kiwango cha kubadilisha pesa ndani ya wiki hii,” alieleza ACP Awadh.
Sambamba na hayo alisema kati ya noti hizo kuna baadhi ya noti zinafanana namba ikiwemo AB26642655J B2 ambazo zipo 40, AB95218841E B2 ambazo zipo 79 na AB262868281 B2 ambazo zipo 114.