NA HANIFA SALIM, PEMBA

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Leila Mohamed Mussa, alisema, Serikali awamu ya nane ipo tayari kufanya kazi na jumuiya za ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kukuza uchumi.

Alisema, lengo ni kukuza maendeleo ya kiuchumi na kuondoa changamoto mbali mbali zilizopo, ndani ya nchi yao, hivyo aliziomba jumuiya kujitokeza kufanya kazi na Zanzibar, ili kuendelea kudumisha utamaduni na urithi wao.

Aliyasema hayo, alipokua akifungua kongamano la uhifadhi wa mambo ya kale na utalii Kisiwani Pemba, lililoadaliwa na jumuiya ya uhifadhi urithi, lililofanyika katika ukumbi wa Green Folliage Mgogoni Chake chake.

“Jitihada zilizochukuliwa na jumuiya hii ni nzuri na sisi serikali tumeunga mkono, nataka niihakikishie jumuiya hii na nyengine iwe ya kitaifa, kimataifa serikali ipo tayari kufanya kazi lengo letu ni kukuza maendeleo ya kiuchumi,” alisema.

Alieleza kuwa, Pemba bado utamaduni wake upo kwa asilimia kubwa hivyo, ni vyema kwa jumuiya zinapotaka kufanya kazi kuendana na utamaduni asilia uliopo, ili kutengeneza vijana wanaoendana na utamaduni wao.

Aidha alisema, katika kulinda usalama wa wananchi, wadau na jumuiya zote nchini zina jukumu la kusimamia na kuchukua tahadhari ya hali ya juu kujikinga na Ugonjwa wa Corona ambao umeikumba Dunia kwa sasa.

Katibu Mtendaji wa tume ya Taifa UNESCO ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Khamis Malebo alisema, tume hiyo ina wajibu wa kuratibu, kusimamia, kutimiza na kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendeleza kutumia urithi wa nchi.