NA MWINYIMVUA NZUKWI

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeeleza kuwa itaelendeleza mashirikiano na mahusiano yaliyopo na wanajumuiya ya Wapikistani wanaoishi Zanzibar kwa manufaa ya Zanzibar na Pakistani.

Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 75 ya uhuru wa Pakistani, Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, alieleza nchi mbili hizo zina historia ya muda mrefu inayotakiwa kuimarishwa.

Alisema viongozi waliotangulia wa nchi mbili hizo, walifanya kazi kubwa kuhakikisha zinakuwa huru hivyo ni julkumu la wananchi na viongozi wa sasa kuimarisha uhuru huo kwa kujenga uchumi imara.

Kitwana alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Pakistani kuja kuwekeza Zanzibar kwa kuwa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, imerahisisha mifumo ya uwekezaji kuvutia wawekezaji katika Nyanja mbali mba;li za kiuchumi na kijamii.

“Zanzibar ina mwingiliano mkubwa na watu wenye asili ya Pakistani, hivyo nawaomba nyinyi wenyewe mliopo hapa au ndugu zetu waliopo Pakistani, kutumia fursa kuwekeza miradi itakayoimarisha uchumi wenu na mataifa yetu kwa ujumla,” alieleza Kitwana.

Aidha aliwapongeza viongozi, wananchi na wana Jumuiya ya Wapakistani wanaoishi Zanzibar kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa nchi yao akieleza kuwa pia ni furaha ya wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake Balozi mdogo wa Pakistani nchini Tanzania, Muhammad Azan Bihan, alieleza kufurahishwa kwake na jinsi nchi yake na Tanzania zinazovyoendeleza uhusiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 75 ya uhuru wake, Pakistani imepiga hatua mbali mbali za kimaendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa jambo linalotoa fursa kwa wananchi wake kujiendeleza.

Akisoma ujumbe wa Rais na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Balozi Bihan alieleza hatua mbali mbali ambazo nchi hiyo imechukua katika kuimarisha ustawi wa jamii na uchumi wa Pakistani.

Alisema kwa wakati tofauti serikali ya nchi hiyo imefanya mapitio ya sera na mifumo ya kiuchumi jambo lililochangia ukuaji wa kasi ya uchumi wa nchi hiyo hususan katika sekta ya kilimo, teknolojia na maendeleo ya jamii.