NA LAYLAT KHALFAN

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imeombwa kuhakikisha upatikanaji wa maslahi bora ya walimu kama moja ya njia za kuimarisha ubora wa elimu nchini.

Akifungua mafunzo ya kitaalamu kwa walimu katika skuli ya msingi Uroa, wilaya ya Kati Unguja, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU), Haji Juma Omar, alisema ili kuongeza ubora wa elimu,  walimu wanapaswa kutunzwa ili kuzalisha wataalamu wa baadae.

Alisema walimu wengi Zanzibar wana hali ngumu hivyo ni vyema kuandaliwa maslahi mazuri ili kuwaongezea kasi na ari ya kufanya kazi kukuza sekta ya elimu hapa nchini.

“Ili taifa liendelee jambo la mwanzo ni kuwekeza kwenye elimu kwani huwezi kuwa na elimu bora kama hakutokuwa na walimu bora,” alisema.

Alisema wakati umefika sasa kwa serikali kuhakikisha inayafanyia kazi malalamiko ya walimu ili ufanisi wa walimu bora uweze kufikiwa.

“Licha ya kuwa mnadai haki zenu lakini ni vyema wajibu wenu kuendelea kufanya kazi kwa moyo mmoja wakati jitihada za kufuatilia maslahi yenu zinaendelea,” alisema.

Aidha Katibu huyo aliyeteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo, aliwataka wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao na kuhakikisha wanakwenda skuli kama inavyotakiwa na kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa.

Naye Mwenyekiti wa Kanda ya Unguja, Daudi Mohammed Ali, aliwataka walimu kuwa wabunifu pale wanapotekeleza majukumu yao ya kazi ili kuwa mfano bora kwa utoaji wa elimu nchini.

Akiwasilisha mada kuhusiana na utoaji wa huduma kwa wanachama, Mjumbe wa Kamati Tendaji Taifa, mwalimu Mohammed Yussuf Mnemo, alisema ZATU inajitihidi kuwaelimisha wanachama wake sheria za kazi kupitia semina za mwisho wa wiki na mafunzo kwa wanachama wakiwemo walimu wawakilishi.

Akitaja baadhi ya sheria hizo ni kuwa ni pamoja na sheria za kazi, sheria za mahusiano kazini, sheria za mfuko wa hifadhi ya jamii (ZSSF), kanuni ya utumishi wa umma na mikataba ya kazi ya kimataifa ili kuwajengea uelewa.