NA NASRA MANZI, WHVUM

WAZIRI wa Habari Vijana ,Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amesema Serikali kupitia Wizara hiyo imetenga  fedha Shilingi bilioni saba kwa   ajili ya vijana kujiwezesha wenyewe.

Akizungumza mara baada ya matembezi yaliyoambatana na mazoezi ya umoja wa Vijana Mkoa wa Mjini (UVCCM) yaliyoanzia Aman hadi katika viwanjan vya maisara KMKM Mjini Unguja.

Alisema lengo la serikali kutenga bajeti  hiyo, ni kuwawezesha  vijana katika shughuli mbali mbali za kujiinua kiuchumi na kupata maendeleo.

Aidha, aliwataka vijana  kuchangamkia fursa na kutochagua kazi ya kufanya, kwani Serikali imetenga  bajeti, ili kuwainua kiuchumi na kupunguza malalamiko.

Alisema  Wizara  pia imejipanga vyema  namna ya kubuni miradi na kuwawezesha vijana pamoja na mabaraza mengine,  ili  kufanya biashara ,Sambamba  na kuwatafutia soko kwa lengo  wanachozalisha kuleta tija kwa kuepusha upotevu wa fedha na kuepusha  kuitia  hasara serikali.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana  Mkoa wa Mjini Kamaria Suleiman, alisema wataendelea na mazoezi katika kuhakikisha umoja vijana UVCCM unakua imara na kujenga Afya zao.

Alisema agizo hilo la kufanya mazoezi kutoka kwa Katibu Mkuu UVCCM Taifa, litakuwa endelevu na kuwafanya Vijana kufanya Kazi kwa umoja na mshikamano katika majukumu yao.