NAIROBI, KENYA

SOMALIA na Kenya zimekubaliana kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati yao uliokuwa na taabu, kufuatia mkutano wa maofisa wa ngazi ya juu wa pande mbili.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa, Rais Mohamed Farmajo wa Somalia, Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble na Waziri wa Mambo ya nje Abdirazak Mohamed walifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Raychelle Omamo mjini Mogadishu ambapo waliazimia kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kiusalama na kidiplomasia.

Nchi hizo mbili zilikubaliana kuandaa haraka kikao cha tatu cha kamati ya pamoja ya ushirikiano kati ya Somalia na Kenya.

Kikao hicho kitaziwezesha nchi hizo mbili kufanya mjadala wa pande zote na kuendeleza njia za wazi za kutekeleza ahadi kuhusu uhusiano wa kidiplomasia, biashara, uwekezaji, usalama, utalii na uchumi.

Waziri Mkuu wa Somalia Roble alisema, baadaye atafanya ziara rasmi huko Nairobi ili kuimarisha zaidi uhusiano na Kenya.

Somalia ilivunja uhusiano wake na Kenya mnamo Disemba 2020 baada ya kuituhumu Kenya kuwa inaingilia mambo yake ya ndani, tuhuma ambazo Nairobi ilikanusha.Somalia ilirejesha uhusiano wake na Kenya Mei 5 kufuatia upatanishi wa Qatar.