KHARTOUM, SUDAN

SERIKALI ya Sudan na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wametia saini hati ya makubaliano (MoU) juu ya utoaji wa habari na utambuzi wa haki kwa wahanga wa mzozo katika mkoa wa Darfur nchini Sudan.

Waziri wa Sheria wa Sudan Nasredeen Abdelbari alisaini makubaliano hayo na Mwendesha Mashtaka wa ICC Karim Khan.

“MoU inasaidia katika kutoa habari iliyoombwa na kuendelea kufanya kazi na waathirika, manusura na asasi za kiraia,” Khan alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Khartoum.

Khan alisema ujumbe wa ICC uliokuwa ukimtembelea na serikali ya Sudan walishindwa kukubaliana tarehe maalum ya kumkabidhi Rais Omar al-Bashir na washukiwa wengine kwa Mahakama, na kuongeza kuwa ICC itafungua ofisi ya kudumu huko Khartoum.

Mahakama ya ICC inataka Sudan imkabidhi al-Bashir na wasaidizi wake wawili wakuu kwa Mahakama ili washitakiwe, akiwashutumu kwa madai ya kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mkoa wa Darfur.

Baraza la mawaziri la Sudan liliidhinisha rasimu ya sheria ya kujiunga na Mkataba wa Roma wa ICC, lakini sheria hii haitofanya kazi mpaka iidhinishwe na bunge la mpito.

Mamlaka ya mpito nchini Sudan, ambayo ilianzishwa baada ya kuondolewa kwa al-Bashir mnamo Aprili 2019, hapo awali wameelezea utayari wao kushirikiana na ICC kuhusu kesi ya washukiwa wanaotuhumiwa kufanya uhalifu huko Darfur.