WAPENZI wasomaji wetu leo tena katika safu hii ya mapishi tunaendelea kuwaletea mapishi mwanana ambayo yatakuwezesha kubadili mlo na kufanya kujiona mpya katika mapishi wewe na familia yako.

Hivyo basi leo nimewatayarishia upishi wa Supu Ya Mahindi, Karoti Na mbatata ambapo unaweza kula bila ya kutowea kitu au unaweza kutoweya mkate wa aina yoyote hasa ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa kiburudishaji kama ilivyo juisi au kimiminika chengine.

Ili basi uweze kuipika supu hii mahindi, keroti na mbatata lazima uwe na vitu hivi vifuatavyo.

VIPIMO

Karoti (katakata ndogo ndogo) – 3

Mbatata katakata vidogo vidogo – cubes) – 3

Mahindi (chembe) – 2 vikombe

Supu ya vidonge (stock – Maggi cubes) – 1 kidonge

Pilipili manga – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – 1 kijiko cha chai

Siagi au mafuta – 2 vijiko vya supu

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

  1. Tia siagi au mafuta katika sufuria, kaanga mbatata, vikiwa karibu na kuwiva tia karoti, endelea kukaanga kama dakika tatu hivi.
  2. Tia mahindi changanya vizuri katika moto mdogo.
  3. Tia maji kiasi, tia kidonge cha supu (Stock), tia pilipili manga, chumvi na ndimu
  4. Acha ichemke hadi mbatata na karoti ziwive vizuri.
  5. Saga nusu yake katika mashine ya kusagia (blender) urudishe ndani ya sufuria. Changanya pamoja.
  6. Mimina katika bakuli ikiwa tayari.