NA MADINA ISSA
TAASISI ya Jakaya Mrisho Kikwete, imesema itaendelea kuiunga mkono serikali katika kuhakikisha mfumo wa huduma ya afya visiwani unakuwa imara ili jamii iweze kuwa na afya njema.
Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, Vanesa Anyoti, aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa siku mbili kwa wadau mbalimbali wakiwemo kutoka wizara ya Afya na Fedha na Mipango Zanzibar juu ya kuanzishwa bima ya afya ya wote.
Alisema, taasisi hiyo inasaidia wadau mbalimbali katika kuhakikisha michakato wanayoiandaa inafanikiwa kwa wakati uliopo kwa watu wote.
Alisema, kusaidia kupata taaluma na uzoefu wa wadau waliokuwa washawahi kufanya kazi ya huduma ya bima ya afya katika nchi mbalimbali ili kujua namna ya kufanikiwa katika suala hilo.
“Baada ya kikao tutahakikisha kwamba kweli mwisho wa mwaka huu wazanzibari wote wanaweza kupata bima ya afya kwa watu wote” alisema.
Hivyo, alisema siku hizo mbili watakaa na serikali kupitia wizara ya Afya Zanzibar na wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar kuona zitatosha kuandaa mpango wa kuwaonesha nini kinafuata baada ya kikao hicho.
Sambamba na hayo, alisema kuwa baada ya kikao hicho wataona nini kinafanyika kupitia serikali na kuamua nini kinataka na jinsi gani wadau wataweza kuisaidia serikali.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee jinsia na watoto, Dk. Abdallah Suleiman, alisema wizara ya afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wapo katika mpango wa kuelekea huko ambapo kwa sasa wapo katika utaratibu wa kupata fikra na mawazo ili kuweka sawa mfumo mzima.
Alisema uzoefu unaonesha kuwa nchi zinazotumia mfumo wa huduma za afya wananchi wao wanapata huduma bora ambapo mfuko wenyewe umekuwa ukijionesha kwani huweza kununua vifaa tiba, dawa na vitu vinavyohitajika kwani mchango unapatikana.
Sambamba na hayo, alisema kuwa utaratibu wa kutolea huduma bure kwa hospitali za serikali unaendelea na haujasitishwa kwa sasa hivyo, alisema mfumo huo wa bima pia utazingatia wananchi wasiokuwa na uwezo ambapo tafiti zitatumika ili kuona namna gani wataweza kuuendesha mfumo huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa ushirikiano wa Kimataifa, balozi wa Uswizi Tanzania, Leo Nascher, ofisa masuala ya Afya katika ubalozi wa Uswizi Tanzania, Esther Majani, alisema, ubalozi huo umekuwa na uhusiano wa muda mrefu na serikali ya Tanzania na Zanzibar na kusema kuwa wataendelea kuunga mkono na kusaidia mageuzi katika mfumo wa huduma ya afya.