NA NASRA MANZI, WHVUM

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita ameliagiza Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kutathmini maendeleo ya ufasaha wa matumizi ya lugha ya kiswahili.

Waziri huyo alieleza hayo jana kwenye hafla ya kulizindua Baraza la saba la Kiswahili Zanzibar, iliyofanyika katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo mjini Zanzibar.

Alisema lugha hiyo ni kielelezo cha utamaduni na maisha ya wazanzibari ambapo Baraza hilo lina jukumu la kutathmini maendeleo ili kuepuka kuzungumza na kuandikwa isivyotakiwa.

Waziri Tabia alisema kiswahili mbali ya kuwa ndio lugha mama kwa wananchi wa Zanzibar, lakini kimekuwa lugha ya dunia hasa ikizingatiwa kuwa kinazungumzwa na kusomeshwa katika nchi mbalimbali ulimwenguni.

Alifahamisha kutokana na hali hiyo, BAKIZA kwa kutumia wataalamu wake ndiyo chombo pekee chenye jukumu la kuhakikisha lugha hiyo inazungumzwa na kuandikwa kwa ufasaha ndani na nje ya Zanzibar.

Tabia alieleza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane, ina dhamira ya kuhakikisha lugha hiyo inakuwa zaidi hasa nje ya mipaka ya Tanzania kwenda mbali duniani.

Alisema katika kufikiwa kwa azma hiyo, serikali itaandaa programu zitakazosaidia kuendelezwa kwa lugha ya kiswahili na kusisitiza kuwa ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 inasisitiza umuhimu wa kuchukuliwa juhudi za kuhakikisha kiswahili kinakuzwa na kuendelezwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Alivitaja vipaumbele vikuu vya ilani ni pamoja na kukuza uchumi wa kisasa fungamanishi, jumuishi na ushindani utakaojengwa kupitia viwanda, huduma za kiuchumi, miundombinu wezeshi itakayorahisisha diplomasia ya kisiasa kiuchumi na utamaduni na kuifanya lugha kutumika kikamilifu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Khamis Abdalla Said alisema anaamini Baraza hilo litafanyia kazi majukumu yake kwa uweledi.

Naye Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar, Dk. Mwanahija Ali Juma alisema Baraza la Kiswahili linafanya kazi kwa sheria namba 4, ya mwaka 2004 ya Baraza la Wawakilishi ambapo kupitia sheria hiyo kazi mbali mbali ziliainishwa ikiwemo, kutoa elimu kupitia redio na televisheni, kutoa mafunzo, semina, uhariri na tafsiri.

Alisema kazi nyengine ni pamoja na kuandaa na kuchapisha machapisho mbali mbali pamoja na kuandaa mashindano ya kukuza na kuendeleza vipaji vya waandishi chipukizi na kuwaenzi waandishi wakongwe.

Pia alisema Baraza la Kiswahili limefanikiwa kuendeleza na kukuza lugha ya Kiswahili kwa kufanya shughuli kwa kushirikiana na taasisi ya uchapishaji, tafsiri, makongamano na kuandaa istilahi.

Alieleza licha ya mafanikio Baraza linakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa jengo kulingana na wingi wa watendaji, udogo wa maktaba ambao unazuia kutolewa huduma ipasavyo. pamoja na ufinyu wa soko la kuuzia machapisho.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili, Saade Said Mbarouk alisema serikali kupitia wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo ina mikakati imara ya kuhakikisha inasimamia ustawi wa lugha ya kiswahili nchini kwa kuwa na udhubutu wa kushirikiana na wadau kwa kuendeleza kiswahili.