NA ABDI SULEIMAN

WAZIRI wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulidi Mwita, amewataka wasanii wa vikundi vya sanaa Pemba, kuhakikisha sanaa hiyo inarithishwa vijana ili kuendelea kudumu.

Alisema sanaa nyingi zinapotea kutokana na wazee kushindwa kuwarithisha vijana wao, jambo ambalo linapelekea sanaa hizo kupotea siku hadi siku.

Waziri Tabia aliyaeleza hayo katika hutuba yake wakati wa mashindano ya vikundi vya sanaa Pemba, yaliyofanyika uwanja wa Michezo Gombani Chake Chake Pemba.

Aidha alisema wizara itahakikisha inakamilisha yale yote yanayohitajika katika kuimarisha sanaa za utamaduni zikiwemo ngoma za asili, ili ziweze kuendelea kubaki katika asili yake na kurithishwa kwa vizazi vya sasa vilivyopo bila ya kupoteza asili yake.

“Tayari sisi kama wizara tumeanza kuchukua hatua za kuviimarisha vikundi mbali mbali vya sanaa, kwa kuandaa matamasha na mashindano mbali mbali ya asili” alisema.

Hata hivyo alisema wizara itaendelea kuimarisha kitengo cha haki miliki, ili wasanii waweze kupata haki zao wale ambao wataweza kuzisajili sanaa zao.

Naye Katibu Mkuu Wizara hiyo Fatma Hamad Rajab, alisema Wizara imejipanga kuleta mabadiliko makubwa katika sanaa, hivyo aliwataka wasani kutoa mashirikiano yao ili kufanikisha malengo ya wizara ya kuboresha sana.

Kwa upande wake mmoja wa waandaaji wa mashindano hayo Ibrahim Bukenga, ameitaka wizara kuhakikisha inawasimamia wasanii kulinda utamaduni wa mzanzibari ambao ndio urithi wa Zanzibar.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya vikundi vya sana Msanii Mohammed Kombo (Mwinyi mpeku), aliutaka uongozi wa wizara, kukaa pamoja na vikundi vya sanaa kisiwani Pemba, ili kushirikiana katika kuimraisha sanaa ikiwemo ya ngoma za utamaduni na sanaa za maonyesho.