NA NASRA MANZI, WHVUM

WAZIRI wa Habari,Vijana ,Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita, amesema wizara itaendelea kuthamini, kuelekeza  na kubuni michezo mipya kwa lengo la kuitangaza nchi.

Hayo ameyaeleza wakati wa hafla ya kuirejesha timu ya Wavu (Volleyball) ya Chuoni, ambayo ilikufa kwa miaka mingi.

Alisema Zanzibar imejaaliwa na vipaji lakini pia michezo mbali mbali,hivyo serikali inaendelea kuthamini na kuipa kipao mbele michezo yote,  kwa vijana ili kuibua vipaji  na kupata fursa kupitia mashindano mbali mbali.

“Serikali yenu ipo pamoja na nyinyi wanamichezo tumieni fursa na muendeleze mchezo huu wa Wavu na msiache kufanya mazoezi” alisema.

Alisema wanatambua changamoto zinazowakabili lakini serikali kupitia wizara, watahakikisha changamoto hizo zinatafutiwa kwa mujibu wa taratibu zilizoekwa kwa ajili ya kuimarisha michezo.

Aidha alisema ni vyema kutengeneza mashindano ya nje na ndani katika mchezo huo, ili kusudi kukuza na kuendeleza kwa ajili ya kuepusha kupotea kwa hadhi ya mchezo huo.

Tabia aliwataka wazazi kuwahamasisha na kushiriki michezo watoto huku wakizingatia masomo, kwani ni vitu muhimu ambavyo vitawapatia maendeleo  katika maisha yao.

Wakisoma risala ya timu ya Chuoni Zainab Suleiman alisema kuna sababu ya kufufua tena mchezo huo, kwani serikali ya awamu ya nane ina moyo wa kuendeleza michezo kwa vijana.