KABUL, AFGHANISTAN
KUNDI la Wanamgambo wa Taliban limewataka viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Afghanistan kuhimiza amani wakati wa sala ya Ijumaa jana ambayo ni ya kwanza tangu wapiganaji wake walipochukua udhibiti wa taifa hilo.
Taliban iliwataka maimamu kutumia mahubiri ya ibada ya jana kuhimiza watu kulinda amani na utulivu pamoja na kuwashawishi kutoikimbia nchi hiyo baada ya kuongezeka kwa wasiwasi kwamba utawala wa kundi hilo utakuwa wa kikatili.
Wito wa Taliban unakuja wakati maandamano ya kulipinga kundi hilo yakisambaa kwenye miji mingi nchini Afghanistan ikiwemo mji mkuu, Kabul na kuna ripoti za watu kuuwawa.
Mashuhuda walisema watu kadhaa waliuwawa baada ya wapiganaji wa Taliban kufyetua risasi za moto kwenye mkusanyiko mkubwa katika mji wa mashariki wa Asadabad.
Ingawa kwa jumla hali ni ya utulivu nchini Afghanistan lakini kumekuwa na ripoti za wapiganaji wa Taliban kutumia nguvu kuwadhibiti waandamanaji.