NA MADINA ISSA

WANANCHI wa Kizimkazi wamesema Tamasha la Kizimkazi la mwaka huu limekuwa na faida kwani limechangia maendeleo ya kijiji hicho ikiwemo Kituo cha Afya na nyumba ya Maendeleo ya Kijiji hicho.

Akizungumza na Zanzibar leo, Said Ramadhan Mgeni, alisema tamasha hilo limeleta manufaa kwa wannachi wa Kizimkazi na maeneo ya jirani, kwani miradi ya maendeleo mbali mbali wameipata tokea kuanzishwa kwa matamasha hayo tokea 2015.

Alisema, moja ya manufaa hayo ni ujenzi wa nyumba ya madaktari ambayo kupitia tamasha hilo imemalizika ambapo sasa imekuwa ikitumiwa na madaktari na wamekuwa hawapati usumbufu.

Aidha alisema kuwa pia alikuwa na tatizo ya nyumba ya walimu ambayo kwa sasa wamejengewa nyumba mpya ya kisasa kupitia tamasha hilo.

Alisema katika sekta ya elimu wameweza kuifanyia ukarabati mkubwa wa skuli yao iliyojengwa mwaka 1910 ambayo hivi sasa imefanyiwa marekebisho na imekuwa inavutia na imekuwa skuli yenye kiwango kikubwa.

Hata hivyo, alisema kupitia tamasha hilo, wamepata skuli ya maandalizi mpya ya kisasa ambayo imejengwa na benki ya NBC na kufunguliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan siku ya kilele cha tamasha hilo.

Hivyo, waliomba serikali kuliendeleza tamasha hilo, kwani limekuwa na manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla kwani limekuwa linasaidia serikali katika kuweka vitega uchumi na nyumba za maendeleo pamoja na harakati za kijamii mbalimbali.

Nae, Mustafa Mohammed Haji, alisema, katika tamsha hilo, alisema mwamko wa wananchi ulikuwa mzuri katika tamasha hilo, ambapo wananchi wengi wamejitokeza katioka tamasha hilo.

Aidha alisema kuwa katika tamasha hilo, wameshuhudia masuala mbali mbali ya utamaduni na kuiomba serikali kuendelea kuwaunga mkono wanakijiji hao ili mila na desturi za kijiji hicho ziweze kuendelea.

Tamasha la kizimkazi lililozinduliwa agosti 23 mwaka huu na mke wa rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Maryam mwinyi, lilifungwa rasmi juzi na rais samia ambapo shughuli mbali mbali za kijamii na kiuchumi zilifanyika katika kipindi cha tamasha hilo.