ZRB namna ilivyojitangaza, Yasema baadhi ya changamoto za kodi zatatuliwa
LWawahimiza wafanyabiashara kulipa kodi bila kusukumwa
NA KHAMISUU ABDALLAH
ZANZIBAR kama zilivyo nchi nyengine zinazoendelea, ambazo hadi sasa hazitegemei rasilimali asili mfano wa madini na mafuta, hivyo kodi imeendelea kubaki kuwa ni chanzo muhimu sana katika kuipatia mapato Serikali.
Kodi inatofautiana na vyanzo vyengine vya mapato kutokana na kwamba ni tozo la lazima ambayo kwa anaestahiki anatakiwa alipe kwa usahihi na kwa wakati.
Kodi hutumika kwa manufaa ya wananchi wote katika kupata huduma za elimu, huduma za afya, ulinzi na usalama, ujenzi wa miundo mbinu, pamoja na huduma zote nyengine za Serikali.
Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), ni taasisi ilianzishwa mwaka 1996 baada ya kupitishwa sheria namba 7 ya mwaka 1996 ambayo imeipa mamlaka bodi hiyo kusimamia utekelezaji wa sheria za kodi zinazohusu ukusanyaji wa mapato ya Zanzibar kwa kutoza na kuyakusanya.
Utaratibu wa ulipaji wa kodi pamoja na uanzishwaji wa vyombo vyake vya ukusanyaji wa mapato una historia kubwa duniani.
Kati ya miaka ya 1960 na 1980 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa ikitegemea sana mapato yanayotokana na kuuza karafuu, mbata na mazao mengine ya kilimo hapa nchini.
Mara tu baada ya kuanguka kwa soko la bidhaa hizo katika soko la dunia, serikali ikageukia uchumi wake katika utalii sambamba na kuanzisha mamlaka za utozwahi ushuru na kodi mbalimbali kusudi kujinasua katika uchumi.
Bodi ya Mapato (ZRB) ikiwa ni miongoni mwao na kwamba ilipewa jukumu la kuhakikisha mapato ya serikali yanapatikana kwa kukusanya kodi za ndani ikiwemo kodi ya ongezeko la thamani, kodi ya ushuru wa stempu, kodi za mafuta, ada mbalimbali za uwanja wa ndege na bandarini na mapato ya mawizara ikiwemo kodi ya ardhi.
Lengo la serikali kuweka bodi hiyo kuhakikisha inakusanya mapato na kuingiza katika mfuko mkuu wa serikali kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo ya nchi.
Katika makala haya maalumu inayohusiana na Tamasha la 45 la kimataifa la biashara lililofanyika mwezi uliopita katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar- es – salaam ambapo bodi ya Mapato ilishiriki iliweza kutambulika zaidi hapa Tanzania.
Makala haya ilizungumza na baadhi ya watu na washiriki waliotembelea banda la taasisi hiyo na kusifia namna ya taasisi hiyo inavyofanya kazi zake.
WANAVYOZUNGUMZA WADAU
Wadau mbalimbali waliotembelea katika banda hilo walipongeza bodi hiyo kupitia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa hatua hiyo muhimu ya kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara.
Wanasema maamuzi hayo yaliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa wafanyabiashara na wananchi kuweza kuwaondoshea changamoto hiyo ambayo ilikuwa ni ya muda mrefu.
Abubakar Juma anasema mara nyingi walikuwa wakisafirisha biashara kutoka Tanzania bara kwenda Zanzibar walikuwa wakitozwa kodi hiyo na hata wakifika Zanzibar walikuwa wakitozwa kodi hiyo kwa asilimia 18 na Zanzibar asilimia 15.
“Kwa kweli tumefarajika sana kuondoka hii changamoto ambayo ilikuwa ikitukwaza kwa muda mrefu tunatamani tufanye biashara Zanzibar lakini jambo hili lilikuwa likituathiri kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Nae Feith Kias anasema kuondoshwa kwa ulipaji wa VAT mara mbili kumewapa ari ya kuwa na utayari kulipia kodi mara moja sambamba na kuongeza wigo wa biashara katika kuwekeza visiwani Zanzibar.
Aidha anasema watu wengi walikuwa wapo nyuma katika kufanya biashara na kuweza kutokana na changamoto hiyo ambayo kwa sasa imetatuliwa kwa kiwango kikubwa.
Happiness Mchom alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa uamuzi wake huo ambao kwa kiasi kikubwa umewapa ari wafanyabiashara na wananchi kuwekeza nchini.
BODI YA MAPATO ZANZIBAR (ZRB)
Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Ofisa Elimu kwa mlipa kodi Bodi ya Mapato Zanzibar, Raya Suleiman Abdalla, anasema VAT ilikuwa na malalamiko mengi kwa wafanyabiashara ambao walikuwa wakiilalamikia ZRB kuhusu kulipa kodi pande zote mbili za Muungano.
Anasema mtu akitoa mzigo Zanzibar analipia VAT na hata akitoa mzigo Tanzania bara anatozwa kodi hiyo, changamoto ambayo waliichukua chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi na kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa na utekelezaji wake umeonekana kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022
Anasema ni wakati sasa kwa wafanyabiashara kuitumia fursa hiyo ambayo inatawawezesha kulipia kodi ya ongezeko la thamani ya VAT kwa upande mmoja wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa kweli hapa wafanyabiashara wengi wametupa moyo wa kuja kuekeza nchini kwetu hii inatokana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuona kila hali inaporuhusu kwa kubadilisha sheria na hii tumeliona katika mwaka huu wa fedha kwa kodi ya VAT,” anasema.
Anasema muamko huo kwa kiasi kikubwa utaiwezesha Zanzibar kuongeza mapato yake kupitia sekta ya uwekezaji na biashara.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, inatoa fursa kwa wawekezaji mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara kuwekeza Zanzibar kwa ajili ya kuchangia pato la nchi na tumeliona katika maonesho haya wengi wana shauku ya kuja kuwekeza kwetu,” anabainisha.
CHANGAMOTO
Anabainisha kuwa, katika maonesho 44 miongoni mwa changamoto waliyokuwa wakiitaja wananchi na wafanyabiashara ni kutokuwa na uhuru katika bandari pale wanapoingiza bidhaa ikiwemo gari na kushauri kukaa pamoja ili kulipatia ufumbuzi jambo hilo.
“Kwa hili tumejitahidi kutoa ufafanuzi wa kisheria juu ya kwanini yanafanyika haya na namna ya serikali yetu ilivyodhamiria kuondosha changamoto zote za kodi ili kustawisha biashara baina ya pande zote mbili za Muungano,” anasema.
Sambamba na hayo anawaomba wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi yanapofika maonesho hayo ili waweze kupata elimu ambayo itawawezesha kujua mambo mengi ikiwemo kazi zinazofanywa na ZRB na utofauti wake na TRA.
“Kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 kuna mabadiliko makubwa ya sheria ambazo zinawapa unafuu walipakodi wetu hii ni fursa kwao kujisajili na kuwa walipakodi halali,” alisema.
Nae Ofisa Uhusiano wa Bodi hiyo Badria Attai Masoud anasema lengo la kushiriki katika maonesho hayo ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwani inaonekana bado wananchi wapo nyuma katika elimu ya kodi.
“Lengo letu ni kuona tunaendelea kuwa washiriki wazuri katika maonesho haya ya saba saba kila mwaka lakini pia kutoa elimu ambayo itawasaidia wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla katika kuhakikisha wanaifahamu elimu hii ya kodi ambayo itakuwa ndio dira katika pirika zao za kibiashara za kila siku, na kwakweli wanakuja sana na tunajitahidi kuwafahamisha,” alibainisha.
Aidha Badria anasema lengo la pili kushiriki maonesho hayo ni kupokea malalamiko ya walipakodi kwa ajili ya kuyachukua na kuyafikisha sehemu husika kwa ajili ya kutatuliwa ili kuongeza ari na hamasa katika suala la ulipaji kodi.
Hata hivyo, anabainisha kuwa mbali na malengo hayo pia ni kuyatangaza mabadiliko ya sheria yaliyofanyika kwa kutumia maonesho hayo ambapo wadau wakubwa wanapatikana katika eneo hilo.
Sambamba na hayo anasema pia ushiriki wa maonesho hayo ni kuimarisha uhusiano baina ya tasisi mbalimbali za serikali na wadau wa kodi ili kubadilishana uzoefu wakiwa na lengo moja la kukusanya kodi kwa pamoja kwani ZRB pekee haiwezi kukusanya kodi bila ya mashirikiano ya tasisi za serikali na wafanyabiashara kwa ujumla.
Badria, anawaomba wafanyabiashara kulitumia banda hilo kwa lengo la kupata elimu ambayo itawawezesha kushajihika kwenda kuwekeza visiwani Zanzibar na kuimarika kwa mapato nchini.
Katika hatua nyengine anawasisitiza wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini ambayo yanategemewa katika kuhudumia maendeleo kwa wananchi.
Hivyo, aliwaomba watanzania kufahamu kuwa Tanzania ni moja lakini katika usimamizi wa sheria za kodi kujua kuwa zipo sheria ambazo zinazosimamiwa na TRA na ZRB.
Hata hivyo Badria anaipongeza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika maonesho ya 44 ikiwemo upatikanaji wa vitambulisho kwa washiriki wa maonesho hayo na sehemu ya washiriki kutoka Zanzibar.
“Hapa tunaishukuru wizara yetu kwani maonesho ya mwaka jana banda tulilopata lilikuwa dogo lakini mwaka huu tumekaa katika sehemu nzuri kimadhari na hata vitambulisho tumevipata kwa wakati,” anasema.
TAN TRADE
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (Tan Trade), Dk. Ngwaza Kamata Soko, anasema maonesho hayo yana manufaa makubwa kwa tasisi za serikali na wajasiriamali kuweza kujitangaza kusoma, kujifunza na kupitia maonesho hayo.
Anasema pia maoensho hayo yanatoa fursa ya wajasiriamali kuweza kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali wenzao wa Tanzania bara na kuweza kutengeneza bidhaa ambazo zinazoweza kupata soko kubwa nje ya nchi.
“Kitendo cha kushiriki katika maonesho haya na maonesho mengine yanayofanyika nchini basi ujue unafunua upeo wa kujifunza na kupata taaluma na kukua kiakili tumeona sasa wajasiriamali wa Zanzibar wamebadilika hasa katika biashara zao totauti na miaka ya nyuma,” alisema.
Hata hivyo, anazipongeza tasisi serikali na wajasiriamali wa Zanzibar kushiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kujitangaza ndani ya Tanzania na nje ya nchi.
“Tunao wajasiriamali mbalimbali hapa wanaotoka Zanzibar ukiacha wale ambao wanauza viungo wapo pia wajasiriamali wanaouza dagaa la Zanzibar ambalo limefungwa vizuri, tunaamini hii ni fursa ya kupata soko la ndani na nje ya nchi,” alisema.
Anasema, pamoja na Tanzania kupata janga la mripuko wa maradhi ya korona lakini Tan Trade ilihakikisha inatumia bidii, uweledi na taaluma kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika na yanafanikiwa kama yalivyopangwa.
Akizungumzia ushiriki wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) katika maeonesho hayo, anasema ushiriki wao utaendelea kujenga urafiki kati yao na tasisi nyengine za Tanzania bara.
KUFUNGULIWA MAONESHO YA SABASABA
Mapema Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akifungua maonesho hayo anasema serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuviwezesha viwanda vidogo na vya kati kukua na kufanya kazi kwa tija,
Anasema ili nchi iweze kuwa na mafanikio makubwa, taasisi za kifedha hazina budi kuweka mikakati ya kutoa huduma ya mikopo rafiki ili kuwezesha ukuaji wa viwanda kwa kuzingatia viwanda vidogo na vya kati ikiwemo vinavyoratibiwa na SIDO katika kila mkoa.
“Taswira hii ya maendeleo ya sekta ya viwanda inafanana na taswira ya maendeleo ya viwanda katika nchi karibu zote duniani,” alisema.
Hivyo, aliwasisitiza wafanyabiashara na tasisi za serikali kuendelea kushirikiana kwa kushiriki katika maonesho hayo ili waweze kujitangaza zaidi.
KUFUNGA TAMASHA LA BIASHARA SABASABA
Akifunga maonesho hayo Makamu wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla anaipongeza wizara ya bishara na maendeleo ya viwanda Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya viwanda Zanzibar natasisi za sekta za umma na binafsi kwa Zanzibar na Tanzania bara walishiriki kwa karibu katika maonesho hayo.
Hemed anasema lengo la serikali ni kuhakikisha fursa zilizokuwepo katika sekta ya biashara, viwanda na uchumi zinatangazwa na kuendelezwa ili kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi kwa ajili ya biadhaa zinazozalishwa Tanzania.
Anasema, maonesho hayo yana faida kubwa kwani maendeleo na mabadiliko ya maendeleo ya bidhaa zinazozalishwa Zanzibar hasa ubora na vifungashio ni hatua kubwa ya kuelekea katika uchumi wa viwanda nchini na fursa za ajira.
Aidha anasema mabadiliko hayo yanatokana na jitihada za serikali katika kuwawekea mazingira mazuri wajasiriamali wake kuona wanazalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitaweza kuuzika ndani na nje ya Tanzania.
Anasema uchumi wa viwanda unamuhitaji kila mmoja kwa bidii na tija hasa katika kipindi hichi ambacho Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kipato cha kati.
Makamu Hemed anatoa rai kwa vyuo vya elimu ya juu, tasisi za elimu na vyuo vya mafunzo mbalimbali kufanya tathmini ya kina ya mahitaji halisi ya rasilimali watu kwa kuzingatia ujuzi na maarifa yanayohitajika katika sekta zote nchini ili ziweze kuzalisha mahitaji halisi ya rasilimali watu kwa kuzingatia maendeleo ya viwanda nchini.
Anasema jitihada hizo zilenge kutatua tatizo la ajira na kuwapunguzia gharama wenye viwanda na wawekezaji kwa kuhakikisha wanapatikana wafanyakazi wenye sifa stahiki.
Alitumia fursa hiyo, kuwapongeza wafanyabiashara wote hasa wa Zanzibar kwa kuitikia wito wa kuyatumia vyema maonesho hayo ambayo yataweza kuwatangaza kupitia mataifa mbalimbali duniani.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban akizungumza katika hafla ya ufungaji wa maonesho hayo anaahidi kuwa wataendelea kushirikiana na TAN TRED ili wafayanbiashara na tasisi za serikali kuona zinapata muamko wa kushiriki maonesho hayo.
Alisema lengo la wizara zao ya SMZ na SMT ni kuhakikisha malengo makuu ya kuanzishwa wizara hizo yanafanikiwa ili ukuaji wa sekta za viwanda na biashara katika nchi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yanafikiwa katika dira zake zote ikiwemo ya 2025 na 2050 ya Zanzibar.
Hata hivyo alibainisha kuwa washiriki kutoka Zanzibar kwa mwaka huu katika maonesho hayo wameongezeka kutoka washiriki 52 na kufikia zaidi ya 66 kwa mwaka huu.
“Hii ni ishara tosha kwamba wafanyabiashara, wajasiriamali na wenye viwanda kutoka Zanzibar wanayaona kwamba maonesho haya kama ni sehemu ya fursa ya kutangaza bidhaa zao na hata tasisi za umma kubadilishana uzoefu katika maeneo wanayofanyia kazi kwa tasisi za Umma kwa upande wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zaidi ya wananchi 700 wametembelea banda hilo na kupata elimu juu ya kazi zinazofanywa na bodi hiyo wakiwemo mabalozi mbalimbali wanazoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania ambapo kauli mbiu ilikuwa uchumi wa viwanda kwa ajira na biashara endelevu.
Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ni tasisi inayoshiriki kwa mara ya tatu maonesho ya tamasha la kimataifa la 45 la biashara tokea yaanzishwe jijini humo mwaka 1976.