ADDIS ABABA, ETHIOPIA

VIKOSI vya waasi kutoka mkoa uliokumbwa na vita kaskazini mwa Ethiopia wa Tigray, vimeushutumu Umoja wa Afrika kwa kufanya upendeleo, siku chache baada ya Jumuiya hiyo kumteua rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, kuwa mpatanishi katika mzozo huo.

Msemaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF, Getachew Reda,alisema umoja huo unaupendelea upande wa serikali ya Ethiopia na kwamba si busara kutarajia ujumbe huo mpya kuleta mafanikio.

Jumuiya hiyo ilitangaza uteuzi wa Obasanjo na kusema ni sehemu ya harakati ya kukuza amani, usalama, utulivu na mazungumzo ya kisiasa.

Mkoa wa Tigray umekumbwa na machafuko tangu mwezi Novemba, wakati waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipovituma vikosi vya shirikisho huko Tigray kwa ajili ya kukiondoa chama cha TPLF.