NA ABDI SULEIMAN

KLABU zinazoshiriki ligi daraja kwa kwanza kanda ya Pemba hatua ya nane bora, zimeendelea na msimamo wao wa kutocheza ligi hiyo hadi pale matakwa yao yatakapotekelezwa.

Miongoni mwa matakwa hao ni kutaka kuonana na rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar kusikiliza malalamiko yao.

Zanzibar leo ilifika katika uwanja wa Gombani saa 9:15 za jioni, nakukuta uwanja ukiwa hauna watu, huku Machomanne na New Stone Town zikishindwa kufika uwanjani hapo.

Pia timu  za Wawi Star na Selem View nazo zilishindwa kucheza licha ya waamuzi kufika uwanjani, huku sababu kubwa ikidaiwa kuwa klabu zinaendelea kusimamia msimamo wao kutokucheza ligi hiyo.

Msimamo wa klabu hizo ulitolewa katika kikao cha pamoja baina ya viongozi wa timu hizo na watendaji wa ZFF Pemba, kilichofanyika Agosti 4 mwaka huu katika uwanja wa Gombani.

Klabu hizo zilipaswa kucheza ligi hiyo ili kutafuta timu moja kutoka Pemba, kuungana na timu 11 za Unguja kwa ajili ya kucheza ligi kuu ya Zanzibar msimu wa 2021/2022.

Katika hoja za klabu hizo zilidai kuwa, rais huyo tangu kuingia madarakani ameshindwa kuonana na klabu za Pemba, huku zikiendelea kusimamia msimamo wao wa kutocheza ligi.

Aidha walidai kuwa mbali na hilo,pia jingine ni kushindwa kutekelezwa kwa makubaliano yao na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, walipokutana mwanzoni mwa mwaka huu.

“Katika makubaliano yetu matano moja tu ndio lililotekelezwa, la kuondoka kwa rais wa shirikisho aliyejiuzulu, lakini mengine bado mpaka sasa hakuna lililofanyika”walisema.