NA MWANDISHI WETU, OMKR

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema chama hicho kimeingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa nia ya kutetea maslahi ya Zanzibar na kuleta maendeleo ya watu wote.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliyasema hayo Tumbatu, alipozkuwa akizungumza na wananachama na wazee wa chama hicho katika ziara rasmi ya kujitambulisha  katika jimbo hilo.

Alisema  ACT kushiriki katika serikali kulitokana na hekima na  maauzi  ya chama na kwamba kazi ya kusimamia suala hilo aliyokabidhiwa ni jambo kubwa na ataifanya kwa juhudi na hekima kubwa ili wananchi wanzanzibar waweze kupata maendeleo.

Aliongeza kwamba kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kuwemo katika serikali kwani ni moja ya njia ya kuhakikisha haki za wananchi zilizomo kwenye katiba zinapatikana na kwamba atatimiza wajibu na jukumu alilopewa katika kusimamia haki hiyo kwa uwezo wake wote.

Hata hiovyo, aliwataka wananchi kuwa kitu kimoja na kuungana pamoja katika kushirikiana na viongozi kwa nia ya kujenga nchi yao.

Kuhusu Suala la Muungano, Othman alisema kwamba kudai  haki za Wazanzibari ni wajibu muhimu unaotekelezwa na viongozi  na kwamba ACT Itaendeleza juhudi ya kuzidai kwa nia ya kurejesha hadhi ya Zanzibar ndani ya mungano.

Aliwataka wananchi na viongozi kutovunjika moyo badala yake waendelee kuunga mkono jitihada za viongozi wao ili kuhakikisha maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano yanazingatiwa.

“Nitachotaka mufahamu kwamba suala la Serikali ya Umoja wa kitaifa sio jambo geni, mataifa mengi tena makubwa kama vile Uingereza, Ujerumani na kwengineko lakini nyinyi watu wa Tumbatu mnausemi wenu mnasema kwamba ‘kila penye wimbi ndio pana njia,”  alifafanua Othman.

Mapema Othman alikutana na wazee wa Chama cha ACT Jimbo la Tumbatu kwa nia ya kujitambulisha na kubadilishana mawazo kutokana na kukabidhiwa jukumu kubwa la uongozi wa Zanzibar.

Katika ziara hiyo Othman, aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Juma Dunin Haji, Kaimu Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Salim Bimani, Naibu Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Omar Ali Shehe na viongozi wengine wa chama hicho.