WAWAKILISHI wa Zanzibar katika michuano ya Kombe la Kagame, KMKM tayari imeshaaga michuano ya mwaka huu, ikiondolewa kwenye hatua ya nusu na Express ya Uganda.

KMKM iliondolewa kwenye hatua hiyo baada ya kukubali kichapo cha magoli 2-1, ingawa ilionesha kiwango bora kwenye michuano hiyo.
Kuondolewa kwa wawakilishi wetu hao ilikuwa ni kama bahati mbaya kutoka na aina ya ushindani iliyouonyesha tokea mwanzo, ikicheza soka yenye kuvutia na kiwango kwenye hatua ya makundi.

Ingawa wana falsafa ya kiswahili wanasema ayekubali kubali kushindwa si mshindani, ukweli wa maneno hayo yanaweza kukubalika upande mmoja na upande mwengine ikawa tofauti, kulingana na mtazamo wa kila mmoja wetu.

Pamoja na hayo yaliotokea, tunachukuwa nafasi hii kuipongeza KMKM kwa namna ilivyopambana uwanjani, licha ya kupata matokeo ya kuondolewa ambayo sisi kama jamii ya wanamichezo tunaamini yalikuwa sehemu ya mchezo.

Hata hivyo, ni dhahiri kwamba tulikuwa na kiu kubwa ya kupata mafanikio na kuiona timu yetu ikicheza hatua ya juu zaidi ya michuano hiyo yenye hadhi kubwa ngazi ya klabu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Lakini tukichukua hali ya kiujumla, tumekuwa wanyonge katika soka la kimataifa kwenye miaka ya karibuni na ushiriki wetu mara kadhaa umekuwa wa kushindikiza tu.

Kutokana na hali ilivyo ni wazi kwamba michuano ya mwaka huu imeshapita na sasa tunalazimika kusubiri mwaka ujayo tukiwa na mtazamo tofauti na mipango madhubuti zaidi kwa klabu itakayotuwakilisha.
Lakini ukweli unabakia pale pale kwamba tunahitaji kwenda mbali zaidi huku tukiwa na ujasiri wa kuamini kwamba tunaweza kuvuka kutoka hatua tuliyofikia mwaka huu na kusogea mbele zaidi, ikiwemo kubeba ubingwa.

Kinachohitajika hapa kwanza kwa klabu zetu kujitathimni na hali tunayoendelea kuizoea ya kuwa washindikizaji wa kila mwaka bila ya kujali gharama ambazo wanaziingia katika ushiriki wa kimataifa.
Ni ukweli kuwa ushiriki wa kimataifa unahitaji fedha nyingi na kwa klabu za Zanzibar hili ni tatizo jengine na mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia mtafaruku katika hili.

Mara nyingi tunakuwa hatuna mipango thabiti huku soka letu likiendeshwa katika hali iliyokosa muelekeo na dira ya kutuongoza.
Lakini hapa hatukusudii kumnyooshea kidole yoyote yule,bali ni kuangalia njia za kujitathimni na kuelewa wapi tunakoelekea ikiwa hali ya sasa ya soka letu itaendelea hivi ilivyo sasa.

Kwa kipindi kirefu, ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye michuano ya kimataifa haujakuwa mzuri na kumekuwepo na dhana iliyojengeka miongoni mwa mashabiki kwamba sisi ni wa kawaida mno.
Hivyo, tunashauri umefika sasa kwa klabu na wachezaji kujitambua kwamba macho ya mashabiki na wanamichezo kwa ujumla yanawaangalia kwa kile wanachokifanya ndani na nje ya uwanja kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.

Bado Zaspoti tunaamini soka letu linaweza kuleta mageuzi makubwa ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.
Zanzibar yenye mafanikio ya michezo inawezekana ikiwa kla mmoja wetu atatimiza wajibu wake.