NA ASIA MWALIM

WAZIRI wa Kilimo, Maliasili, Umwagiliaji na Mifugo Dk. Soud Nahoda Hassan amesema serikali itaendelea kutoa mashirikiano kwa taasisi zenye malengo ya kuwasaidia wakulima nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri huyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Kilimo cha Umwagiliaji Maji , Haji Hamid Saleh, alisema hayo wakati akifungua mkutano wa kuitambulisha na kujadili fursa za taasisi ya PASS Trust, uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Kiembesamaki Zanzibar.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia wananchi kupata huduma muhimu za kisasa katika kuimarisha sekta ya kilimo na maendeleo ya nchi kiujumla.

Alisema mashirikiano hayo yamekusudia kutoa fursa za maendeleo muhimu ya wananchi na viwanda vya Zanzibar katika kuchangia jitihada za kupunguza umaskini.

Dk. Soud  alisema njia hiyo itasaidia kustawisisha upatikaji wa huduma bora kwa kutumia fursa za uelewa na kuweka mazingira rafiki kwa wakulima ili kuhakisha  uzalishaji mazao ya wakulima unaongezeka.

Aidha alisema serikali inatambua kuwa wakulima  wengi nchini wanashindwa kutumia teknelojia nzuri ikiwemo upatikanaji wa pembejeo hivyo taasisi hiyo itasaidia upatikanji wa nyenzo muhimu  ikiwemo mikopo ya kibenki na taasisi nyengine za kifedha.

“Sekta ya kilimo ni miongoni mwa sekta muhimu na za kipaumbele nchini kutokana na mchango wake katika maendeleo kwa kutoa ajira kwa zaidi ya asilimia 70 ya wazanzibar ikiwa ni pamoja upatikanaji chakula na lishe,” alieleza Dk. Soud.

Alifahamisha kuwa licha ya uzalishaji mkubwa wa baadhi ya mazao nchini sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ya tija ndogo jambo ambalo linaleta usumbufu kwa wazalishaji na wadau wa kilimo kiujumla.