ISLAMABAD, PAKISTAN

UMOJA wa Falme za Kiarabu, UAE umesema unaanza tena kutoa visa za watalii kwa wasafiri wote waliopatiwa chanjo dhidi ya virusi vya korona.

Mpangilio huo umeanza jana, karibu mwezi mmoja kabla ya mji wa Dubai kuwa mwenyeji wa Maonyesho ya Dunia.

Serikali ya UAE inasema wageni bado wanahitajika kufanyiwa vipimo vya lazima wanapowasili. Inatumai kuanza kutolewa tena kwa viza hizo kutasaidia juhudi za kitaifa kufikia ufufuaji endelevu wa uchumi na ukuaji.

Serikali inakusudia kuvutia wageni milioni 25 kwenye maonyesho hayo yatakayodumu miezi sita wakati kukiwa na vizuizi vya kupambana na korona vilivyowekwa na mataifa mengine.

Maonyesho hayo ambayo ni ya kwanza kabisa kuwahi kufanyika Mashariki ya Kati, yamepangiwa kuanza Oktoba 1.

Uchumi wa UAE unategemea mtaji wa kigeni,mji mkubwa zaidi wa Dubai ulianza tena kuwapokea watalii mwezi Julai mwaka jana bila kuwataka kujitenga wanapowasili.

Lakini mamlaka baadaye ziliweka vizuizi vya kuingia kwa wasafiri kutoka baadhi ya nchi, zikiwemo India na Pakistan, baada ya aina ya Delta ya virusi vya korona kuenea mjini humo.