-
Ni rahisi kufuga baada ya kupata ushauri wa wataalamu
-
Yana soko zuri ndani na nje ya nchi
-
Ni utekelezaji wa Uchumi wa Buluu
Na Thureya Ghalib, Idara ya Habari Maelezo, Pemba
NENO Uchumi wa Buluu lilikuwa geni miongoni mwa wananchi wengi wa Unguja na Pemba. Walikuwa wakifahamu mazingira yaliyowazunguka tu ya bahari na katika bahari kazi kubwa ni uvuvi wa samaki na kidogo ukulima wa mwani.
Katika Awamu hii ya Nane imekuja na Sera ya Uchumi wa Buluu , ambayo ni kutegemea bahari katika kuimarisha uchumi kwa njia ya uvuvi, mafuta, ufugaji wa viumbe vya bahari, gesi asilia na mengi yanayohusiana na bahari.
Hivi sasa neno hilo likitamkwa linaleta faraja kwa kila mwananchi wa Zanzibar, kwani wengi hao wanalitafsiri kama ni ukombozi wa kiuchumi unaotokana na vilivyomo ndani ya bahari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi, ameunda Wizara maalum ya Uchumi wa Buluu, ili kuweza kuwasaidia wananachi wake kuinua uchumi wa wao na Taifa kwa ujumla.
Dhamira hiyo haina maana kuwa Rais amezitupa taasisi nyengine na kuegemea uchumi wa buluu pekee ,lahasha bali lengo lake kubwa ni kuwakomboa wananchi wake katika umasikni kupitia nyanja zote.
Katika kampeni zake za kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar katika kiwanja cha Skuli ya Micheweni, Wilayani humo Mkoa wa Kaskazini Pemba, alizungumzia maneno haya:
“Nimekuwa nikizungumzia Uchumi wa Buluu katika hotuba zangu nyingi kwa maana ya utalii, uvuvi, mafuta, gesi na viwanda vinavyotumia malighafi za bahari, lakini haina maana tutasahau kilimo. Bado kilimo kitapewa kipaumbele”, alihutubia.
Kwa mukhtadha huo, wananchi wamekuwa wakiunda vikundi mbalimbali vikiwemo vya ufugaji samaki,majongoo bahari na wakulima wa mwani ikiwa ni muitikio wa Uchumi wa Buluu.
Mwandishi wa Makala haya ameamua kugusia juu ya ufugaji wa majongoo bahari ,ili kufahamu ni kwa kiasi gani wananchi wameitikia na namna gani wanajikumu kimaisha kupitia ufugaji huo.
Mwandishi alililazimika kufanya safari kufuata kikundi cha ufugaji majongoo, ambacho aliambiwa ni safari ya kwenda kisiwani kwa kutumia mashua yenye kukabiliana na mawimbi ya bahari.
Haikuwa safari rahisi mpaka kufika katika kisiwa cha Uvinje, kilichopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ili kupata kiundani utaalamu wa ufugaji wa majongoo ya pwani na namna wana kikundi wanavyofaidika na changamoto zinazowakabili katika ufugaji wa viumbe hivyo vya bahari.
Safari ya Uvinje kwa salama kabisa tulifika na kulakiwa na wanakikundi cha Juhudi na Maendeleo wa Kisiwa cha Uvinje, chenye wanachama 12 wakiwemo akinamama watano na akinababa saba, ambacho kilianzishwa tarehe 16 Septemba,2019.
Baada ya kusalimiana na kujuana wanakundi walimueleza mwandishi wa makala haya kuwa wamehamasika na ufugaji wa majongoo bahari kwa lengo la kujiongezea kipato, jambo ambalo linawasaidia katika kupiga hatua katika maisha yao ya kila siku.
Walieleza kila siku zinapozidikwenda, ndivyo wanavyozidi kuhamasika na ufugaji wa majongoo hayo ,kwani wamekuwa wakipata ujuzi mpya kwa waliotangulia katika ufugaji huo.
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi hao Mwenyekiti wa kikundi hicho Sharif Hamad Haji, alisema kuwa walihamasishwa na mmoja wa mfugaji wa majongoo kutoka kisiwa cha Kojani , na kuelezewa faida na changamoto zake ndipo walipoamua kuanza rasmi shughuli hiyo.
Alifahamisha baada ya kupata taaluma hiyo, walianzisha shamba na kuunda kikundi cha watu kumi na mbili na kuanza ufugaji wa majongoo bahari kwa awamu ya kwanza.
Alisema kwa hatua ya mwanzo walipata kasoro ndogo ndogo katika ufugaji wao, hivyo waliomba msaada kutoka Idara ya Maendeleo ya Uvuvi wawasaidie kuwaongoza, ili kuondoa kasoro hizo.
“Mbali na kuwa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi inachukua jitihada kubwa katika kutupa elimu na kusababisha faida kubwa kwetu,bali tunaomba wazidi kuwepo karibu na sisi kutueleza sheria zao ili tufanye shughuli zetu tukiwa salama,”alieleza mwenyekiti huyo.
Alifahamisha kuwa kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inapenda maendeleo kwa wananchi wake, imechukua jitihada za makusudi kupitia Idara ya Maendeleo ya Uvuvi ikiwa ni pamoja na kufika katika maeneo yetu, kuona mashamba pamoja na kuyachukua majongoo kupelekwa katika maonesho mbali mbali.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na kuhamasika, uzalishaji ukaongezeka na kulazimika kuongeza ukubwa wa shamba kutoka mita ishirini hadi kufikia mita ishirini na saba.
“Tumerefusha mita za kinga (kuta) ambazo zitakinga wale wanaotembea tembea katika eneo la shamba, ili wasituharibie takriban mita 20, “alisema Sharif.
Alifahamisha kuwa Jongoo anaefugwa huchukua muda wa miezi 8 mpaka 12 hadi kukua na kuvunwa kwake, na viumbe hao hawana chakula chochote wanacholishwa isipokuwa chakula chao hufyonza mchanga wa bahari ndimo wanapata chakula.
Alieleza kuna aina nyingi za majongoo bahari wanayofugwa, lakini wao wanayo majongoo meupe au maarufu ‘sandfish’ na walianza na ufugaji wa majongoo 13 na kwa sasa wanao zaidi ya 200.
Akielezea changamoto wananazozipata katika ufugaji huo, mwenyekiti huyo alisema ni ukosefu wa taaluma kwa ajili ya ufugaji wa majongoo hayo na wameiomba Serikali iwaletee wataalamu waje wawafundishe.
Alisema changamoto nyengine ni kukosa fedha za kujikimu kwa kuendesha shamba lao. “Hatuna nyenzo za kurutubisha vizuri mashamba yetu. Fedha hatuna”, alisema Sharif.
Akizungumzia Soko la majongoo, alisema lipo vizuri la ndani na nje, kwani jongoo mmoja huuza shilingi 5,000 na kwa soko la nje kilo moja ni zaid ya shilingi 80,000.
Alisema wao wanauza majongoo yakiwa mabichi, ambapo hadi sasa wanatumia masoko ya ndani tu na hawajawahi kusafirisha nje.
Hata hivyo, alieleza kuwa kwa sasa hawana mpango wa kupanua shamba lao, kwani hakuna mtu ama kiongozi yoyote aliyewasaidia tokea kuanzisha kikundi hicho.
Alifahamisha kuwa katika shamba lao hilo wamewahi kuvuna mara tatu, na pesa walizozipata ziliwasaidia kujikimu kimaisha pamoja na kuendeleza ufugaji wao na kununua nyenzo za kujengea uzio.
“Tumevuna majongoo hayo mara tatu tangu tulipoanzisha kikundi chetu ,na lile lengo la kujikwamua kimaisha limeweza kufikiwa”, alifahamisha mwenyekiti Sharif.
Kwa upande wake mmoja wa mwanakikundi hicho Mboja Juma Makam, alisema lengo la kujiunga na kikundi hicho ni kujikomboa na umaskini.
Alisema tangu ajiunge na kikundi hicho ameweza kufaidika na mambo mengi ikiwemo elimu pamoja na kufahamu faida mbali mbali za ufugaji wa majongoo hayo.
“Kwa sasa naweza kupata mahitaji yangu ikiwemo kusomesha watoto,kupata chakula na mahitaji mengi ya kijami”, alisema.
Kwa upande wa msimamizi wa shughuli za ufugaji wa mazao ya baharini kutoka Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Mohamed Salim Othman, alisema shughuli hizi za ufugaji hapa Zanzibar zimeaanza katika miaka ya karibuni na kwa upande wa Pemba tayari wamekwisha kuhamasika .
Alieleza hii ilifanyika mara baada ya kufanyika takwimu na kuonekana rasilimali yetu ya majongoo baharini imeanza kupotea tofauti na hapo zamani.
Alifahamisha kuwa mara baada ya kuonekana hilo ndipo walipoamua kushajiisha wavuvi ama watu wanaokaa karibu na bahari kuweza kufuga majongoo ili kuyanusuru yasipotee kabisa.
“Jamb lililosababisha kupotea kwa majongoo ni kutokana na kuzidi shughuli za uvuvi baharini ,hivyo tuliwazidi majongoo baharini na kusababisha kuanza kupotea na ikabidi wanapozaliwa wengi hufa kuliko wanaokuwa hai”, alisema msimamizi huyo.
Msimamizi huyo aliendelea kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeamua kuwarahisishia wafugaji kituo cha kuzalisha vifaranga Beit el Raas, ambapo miongoni mwa vifaranga hivyo ni majongoo bahari, kaa na samaki wa mwatiko.
Alisema kuna mambo ya kuzingatia kabla ya kuanzishwa kwa ufugaji wa baharini, hivyo kabla ya ufugaji ni muhimu kuonana na mtaalamu ili aweze kuwapa elimu wafugaji.
Hata hivyo, alieleza ni vyema wananchi wakahamasika na ufugaji wa viumbe bahari, ikiwa ni njia nzuri ya kumuunga mkono Rais wetu wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.