KAMPALA, UGANDA

SERIKALI ya Uganda imeafikia kupokea wakimbizi 2,000 kutoka Afghanistan kufuatia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.

Esther Anyakun Davinia, Naibu Waziri wa Misaada ya Dharura, Majanga na Wakimbizi alisema Rais Yoweri Museveni ameafiki ombi la Marekani la kuwapokea wakimbizi hao.

Davinia alisema Waafghanistan hao watakuwa nchini Uganda kwa muda wa miezi mitatu kabla ya serikali ya Marekani kuwahamishia kwingine.

Hata hivyo, haikujulikana mara moja ni lini wataanza kuwasili.

Kulingana na taarifa ya serikali ya Uganda, gharama zote zitakazotumika kipindi wakimbikizi hao watakuwa nchini zitalipwa na Marekani.

Wakimbizi hao watapewa makaazi nchini Uganda kwa kipindi cha miezi mitatu na watafika katika makundi ya watu 500.

Albania na Kosovo pia zimekubali ombi la Marekani la kuwapokea kwa muda, wakimbizi wa Afghanistan.

Hayo yanajiri wakati ambao Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) imezitaka nchi mbalimbali kuzuia hatua yoyote ya kuwarejesha makwao kwa nguvu wakimbizi wa Afghanistan wakiwemo wale ambao maombi yao ya ukimbizi yamekataliwa.

Marekani iliivamia Afghanistan mwaka 2001 kwa lengo la kuliangamiza kundi la Taliban.

Baada ya kuikalia kwa mabavu ardhi ya Afghanistan kwa kipindi cha miaka 20 imeshindwa kuliangamiza kundi la Taliban ambalo sasa limeshika tena madaraka ya nchi hiyo.

Vilevile katika kipindi hicho cha kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ugaidi umekuwa na kupanuka zaidi, biashara na uzalishaji wa dawa za kulevya umeimarika na maelfu ya Waafghani wameuawa kutokana na machafuko yanayoigubika nchi hiyo.