Watendaji watakiwa kuwa wadilifu, wanachama wajitokeze

NA MADINA ISSA

WATENDAJI waliopewa jukumu la kuhakiki wanachama wa kampuni ya Mastarlife, wamesisitizwa kufuata taratibu zilizowekwa li zoezi hilo liende vizuri na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Akizungunza katika kikao cha kamati tendaji kilichowashirikisha watendaji wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuwia Rushwa na Uhujumi Uchumi Zanzibar (ZAECA), Makarani Ahmed, kilichofanyuika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Vuga mjini Unguja.

Alisema, zoezi hilo linalotarajiwa kuanza leo katika mkoa wa Kaskazini Unguja na litakuwa katika maeneo maalum yaliyopangwa kwa ajili ya uhakiki huo.

Alisema, kamati imejipanga kuwahudumia watu wote walioweka fedha zao katika kampuni hiyo na kueleza kuwa matarajio ya kamati zoezi litakwenda vyema kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kila mmoja apate haki yake.

Aliwataka wanachamawatakaokwenda kuhakikiwa kuchukua vielelezo vyote ikiwemo mikataba waliyojazishwa na kampuni hiyo pamoja na vitambulisho walivyotumia katika ujazaji wa mikataba hiyo ili zoezi liweze kwenda vizuri na kuweza kuwafahamu wahanga husika.

“Imani yangu zoezi hili litakwenda vizuri na lengo kufikiwa ikiwemo kuwapatia stahiki zao waathirika wote kwani serikali imejidhatiti kuona haki za wahanga hawa zinapatikana,” alisema.

Nae, Mwenyekiti wa kamati hiyo, ambae pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mashitaka, Muumin Khamis Kombo, alisema hatua hiyo ni miongoni mwa hatua nyengine ya utekelezaji wa shughuli za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ambapo awali uhakiki wa ndani ulifanyika na sasa wanakwenda kwenye jamii.

Alifahamisha kuwa uhakiki huo ni sehemu ya utekelezaji wa amri ya mahakama ambapo zoezi hilo, litasimamiwa na kuripotiwa kwa mujibu wa taratibu za sheria.

Sambamba na hayo, aliitaka jamii kutoa ushrikiano wakati wa uhakiki huo na kutumia vyema fursa hiyo kwa kuhakikisha azma ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ya kuona kila mmoja anapata haki yake kwa mujibu wa taratibu.