BERLIN, UJERUMANI
KANSELA wa Ujerumani Angela Merkel amesema serikali yake itaongeza misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan kwa Euro milioni 500.
Ujerumani ilikuwa tayari imeahidi kutoa Euro milioni 100 kama msaada wa dharura kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi wa ndani nchini Afghanistan, fedha hizo zikitolewa kupitia mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer alihimiza kufanyike makubaliano na Taliban juu ya kuwahamisha watu zaidi kutoka nchini Afghanistan.
Jeshi la Ujerumani Bundeswehr, tayari limewahamisha watu 3,800 kutoka Afghanistan japo hatma ya kuendelea na zoezi la kuwahamisha watu zaidi haijulikani baada ya Taliban kuingia madarakani.
Awali, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas alionya kuwa hakuna muda wa kutosha wa kuwahamisha watu wote waliowakusudia kutoka Kabul.