Humsaidia mja mara baada ya kufariki (akhera)
Na Asha Maulid (KMWNA)
“AKIBA Haiozi” ni aina ya methali ambayo jamii huitumia sana hasa katika kutanabahisha jambo fulani, lenye maana ya kuwa kitu kilichowekwa au kuhifadhiwa hakiwezi kuharibika, pia methali hii hutumika kwa kumhimiza mtu ajiwekee akiba kwa faida ya baadae.
Hata katika Uislamu nao unathamini mtu kujiwekea akiba, ikiwa kama sadaka ambayo inayowanufaisha watu hapa Duniani na hata baada ya kufariki.
Kwa mnasaba huo uwekaji wa akiba kwa kutoa sadaka ambayo itasaidia kiimani mbele ya Allah (S.W) ni bora zaidi kwani hupata fadhila.
Uwekaji wa mali yoyote kuwa ni Wakfu kimaana ni sadaka inayoendelea ambapo muekaji huiweka katika dhima ya Subhanahu Wataala ili isije kumilikiwa na mtu mwengine.
Kiutaratibu mali ya Wakfu inaweza kuwa mali inayohamishika na isiyohamishika kama vile pesa, Madini yenye thamani, Hisa, Gari na vitu vyengine ama kwa upande wa mali isiyohamishika ni kama vile ardhi, majengo, miti, nyumba za makaazi na viwanja.
Kimsingi hizi ni baadhi ya mali zinazofaa kutolewa ambapo mueka Wakfu ataweka kupitia mali hizo na kwa sharti awe mmiliki mwenyewe na kitu hicho kinachowekwa Wakfu kiwepo.
Mwandishi wa makala hii amezungumzia umuhimu wa mtu kuweka Wakfu kama ni akiba kwa kupitia malengo ya uwekaji Wakfu kama kuleta maendeleleo ya jamii katika kusaidia wahitaji.
Muweka wakfu atasaidia kuchangia uletaji wa maendeleo ya jamii, kupitia upatikanaji wa maji safi na salama kwa kuchimba visima au kwa mtu mwenye uwezo zaidi kujenga barabara au nyumba za makaazi zitakazowasaidia walimu wa madrasa, walimu wa skuli na hata madaktari kwa wanaokaa masafa ya mbali kwa lengo la kuhakikisha ile huduma wanayoitoa maafisa wale iwe nzuri na kwa wakati unaofaa kwa kuleta maendeleo.
Pia kuweka usawa wa maisha ya walio katika mazingira magumu, ikiwa muweka Wakfu atawanufaisha watu wasiojiweza kwa kuwainua kiuchumi.
Kwa mfano mtu ataweka mali yake wakfu manufaa yatakayopatikana kwa kufanyia miradi katika mali ile itasaidia kuwainua wanaoishi katika mazingira magumu kwa awamu.
Mathalan katika nchi za nje kuna nuymba ya makaazi na maduka, iliyoko Wilaya ya Alkhan, Sharja, U.A.E.
Aliyeweka Wakfu ni mtawala wa Sharja, Msimamizi ni Mamlaka ya Wakfu Sharja na Wanufaika wake ni Masikini wa visiwa vya Comoro, tunaona umuhimu wa kuweka Wakfu kwa mtu kupata radhi kwa Allah kama ni sadaka na hata kuinua watu wanaoishi katika hali ngumu.
Kunyanyua viwango vya elimu kwa kufanya kuwekeza katika miradi mbali mbali ikiwa ukodishwaji wa mali husika na kinachopatikana manufaa yake ni kuwanyanyua watoto katika elimu pamoja na kuwasaidia wanafunzi kimakaazi kwa lengo la kusoma kwa utulivu ili waweze kufikia malengo walioyakusudia.
Mfano makaazi ya wanafunzi katika chuo kikuu cha Moulay Ismail, Menes Morocco kimefadhiliwa na APIF (IDB) kwa mkopo wa miaka 30.
Kusimamia nyumba na taasisi za ibada kama misikiti, makaburi, hospitali, umuhimu mwengine wa kuweka Wakfu ikiwa pamoja na kusimamia taasisi zilizoainishwa hapo juu, ambapo kwa hapa Zanzibar asilimia kubwa ya uwekaji wa Waqfu ni kwa taasisi za kiibada kama vile misikiti.
Pia wakfu nyengine ni ambao manufaa yake yanapelekwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu kwa kuwasaidia wagonjwa hao, unaona ni jinsi gani Wakfu ulivyokuwa na umuhimu kwa jamii.
Pia Wakfu unaweza kusimamia vituo vya ustawi wa jamii kama vile vituo vya kulelea mayatima kwa kuwasaidia mayatima hao, muweka wakfu kunufaika mbele ya Allah (S.W).
Malengo yote hayo ya wakfu yatatimia ikiwa mali ambazo zimeekewa Wakfu katika malengo hayo na msimamizi wa mali hizo ni afisi inayojihusisha na masula ya uwekaji Wakfu, kwa kuzisimamia kwa ajili kuzipangisha na wapangaji kulipa kodi kwa wakati na kufanya miradi ya kimaendeleo ambao utawezesha kuhudumia malengo hayo .
Mwandishi wa makala hii, pia amezungumzia namna ya kuweka Wakfu kwa Waislamu wanaotaka kuweka Wakfu, ambapo tunashuhudia watu wengi huwa wanasema nyumba au Shamba hili ni la Wakfu bila ya kujua taratibu za uwekaji za uwekaji wakfu.
Katika uwekaji wa Wakfu kuna namna nyingi za uwekaji kwa kutumia lafdhi zilizo wazi kwa mfano kusema au kuandika nimeweka Wakfu , ikiwa ina maana ya kuwa nimekifunga au nimeisabilia mali yangu hii kwa Allah (S.W), pamoja na kuandamana na nia ya kuweka Wakfu ambapo hapa muweka Wakfu anatakiwa awe na nia ya kuweka Wakfu kwa kupata radhi kutoka kwa Allah (SW)
Kama baadhi ya watu wanataka kuweka wakfu kwa ajili ya kukimbiza mali katika mirathi kwa wale watu ambao wana watoto wakike pekee au watu waliokuwa hawajabahatika kupata watoto kwa kuhofia kuja kurithiwa na watu wengine.
Vile vile, unaweza kukisifu kitu kwa sifa za Wakfu kwa kusema Sadaka hii ni haramu kuuzwa, wala kugaiwa wala kurithiwa, kwa kuzungumza hivyo na kama kutakuwa na mashahidi ambao watasikia kali ile na kuifahamu ni wazi kuwa Sadaka ile itakuwa imeshaekwa wakfu kwa njia ya matamshi.
Wakfu pia unaweza ukawa wa vitendo bila ya kutamka wala kuandika kwa kufanya ishara au kitendo kinachoonesha kuwa ni Wakfu kwa kujenga msikiti , kuchimba visima na kujenga madrasa au skuli kwa ajili ya kuwasaidia wanajamii
Pia, wakfu unazingatia kanuni ya kisheria isemayo “kilichoandikwa ni sawa na kilichotamkwa” hivyo basi yale yote yanayohusiana na maneno ambayo mtu alitamka yatachukuliwa kama ni hukmu ya kuwekwa Wakfu ikiwa yataandikwa rasmi .
Ijapokuwa mali ile itakuwa imeshafungwa kwa ajili ya Mwenyezimungu lakini kwa wakati tunaokwenda nao hivi sasa, ni lazima muweka wakfu atapaswa kuzingatia taratibu nyengine za kisheria ikiwemo kusajili wakfu katika Mamlaka husika ili aweze kupata kinga na haki nyengine kisheria kwa kupatiwa hati ambayo itayoonyesha kuwa mali hiyo ni Wakfu.
Tofauti na kutamka maneno na kuandika kwa kutumia vikaratasi vya mchele ambapo itapelekea migogoro kwa baadhi ya watu wengine kupinga Wakfu ule.
Kuweka Wakfu hakuhitaji mtu kulazimishwa bali ni jambo la hiari , hivyo basi muweka wakfu atapaswa azingatie masharti ya ya uwekaji wakfu ili wakfu wake uwe sahihi ambapo masharti hayo yatamhusu Waqif, mali inayowekwa na utaratibu wa uwekaji Wakfu kama ifuatavyo :
- Aimiliki mali anayoweka Wakfu yaani umiliki wa kisheria, hivyo haifai kuiweka Wakfu mali aliyoipatakwa wizi unyang’anyi, dhulma au hata mali aliyoinunua bila ya kukabidhiwa rasmi.
- Awe mwenye akili timamu Hivyo haisihi kwa mwendawazimu au aliyechanganyikiwa.
- Awe baleghe (hausihi Wakfu wa motto hata kma ni mwenye kupambanua)
- Awe ni mwenye utambuzi kisheria, hausihi Wakfu wa mtu aliyezuiliwa kufanya matumizi kisheria , alyefilisiwa au aliyeghafilika.
- Awe na ni ya dhati kwa kuweka Wakfu kwa hiari yake sio kwa kulazimishwa.
- Malengo ya Wakfu yakubalike kisheria.
Baada ya kuangalia Sharti za anaetaka kuweka Wakfu ni vyema kuangalia nguzo
Kwa mnasaba huo, kwa mtu ambae amekusudia kuweka Wakfu ni lazima azingaite zitimie nguzo zifuatazo:
Muweka wakfu (Waqif) Kwa upande wa muweka Wakfu lazima anatakiwa awe baleghe ,mwenye akili timamu na asiwe amelazimishwa, hapa kinachoangaliwa zaidi ni ile nia iliyokusudiwa iwepo na awe mmiliki halali wa mali inayofaa kuwekwa Wakfu
Kitu au mali inayowekwa Wakfu (Mawquf), ni lazima kitu ambacho kinatarajiwa kuwekwa wakfu kijulikane na kiweze kutumika ni iwe miongoni mwa zile aina za mali zinazofaa kuwekwa.
Pia Wanufaika wa mapato au mali za Wakfu (Mawquf ‘alaihi), Muweka Wakfu anapotaka kuweka huo wakfu, ahakikishe anaonyesha makusdio ya wakfu huo kwa kuwaekea wanufaika wake ambao watanufaika na mapato ya mali iliyowekwa wakfu iwe familia , jamii au hata taasisi.
Mkuu wa kitengo cha wakfu, katika ofisi ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, Sheikh Saleh Rashid Salum, ambayo amepewa dhamana ya kusimamia mali za Wakfu, kuhusiana na usimamizi mzima wa mali hizo za Wakfu zilizochini ya Kamisheni, zinavyosimamiwa hadi wanufaika kupata haki zao.
Sheikh Saleh anaeleza katika usimamizi wa mali kwanza kuhakikisha kuwa mali yenyewe inayosimamiwa iwepo kama ni nyumba au shamba liwe linaleta tija au haileti tija muhimu kuwa kile kitu chenyewe kilichowekwa kiwepo.
Aidha aneleza kuwa katika usimamizi wa mali ya Wakfu kinachoangaliwa ni ile jitihada ya kuitunza ile mali yenyewe ikiwa ni shamba au nyumba mfano.
“Ikiwa ni mashamba ni kuhakikisha kuwa shamba lile linapimwa kwa ajili ya kutambulika mipaka yake linalimwa na kupanda miti mingine ili kuhakikisha shamba lile listawi vizuri.
“Baadhi ya nyumba huwa tunaangalia uimara wa nyumba kwa kuangalia matengenezo na matumizi ambayo yanayotumiwa na wapangaji, tunaona nyumba nyingi za wakfu ni za zamani zina vyumba viwili vya kukaa watu wachache lakini kwa sasa hivi nyumba hizo utakuta wanakaa watu 15 kiasi ambacho nyumba ile haihimili uwezo wa watu wale ukizingatia ni nyumba ya zamani”, alisema.
Alisema Kamisheni ya Wakfu inahakikisha kupunguza idadi ya watu kwa kuepuka uharibifu wa mara kwa mara pindi inapofanyiwa matengenezo.
Vile vile, Mkuu huyo anaeleza kuwa Kuweka wapangaji na kuhakikisha wanalipa kodi inavyotakiwa ni katika usimamizi wa mali za Wakfu.
“Kwa upande wa kodi tunahakikisha kuwa kodi inayolipwa inakidhi kuwalipa wanufaika na kufanyiwa matengenezo ya nyumba, kwasababu kuweka wakfu mali isiyohamishika ni wakfu wa muda mrefu ni vyema kufanya matengenezo ili kuhakikisha uimara wa jengo”.
“Mpangaji hapaswi kubadilisha matumizi ya nyumba bila ya kutoa taarifa kupitia Kamisheni ya Wakfu na ikiona inafaa kwa matumizi hayo anayotaka mpangaji anaruhusiwa na kama hayafai haruhusiwi.
Kwa mfano, alisema kuna baadhi ya wapangaji wanaopanga nyumba kwa ajili ya makaazi na baadae kufanya magodauni kwa ajili ya kuwekea mizigo kufanya hivyo ni makosa kisheria kutokana na nyumba hizo maalum kwa makaazi na zinahitaji zipate hewa.
Alisema, nyumba hizo zinapowekwa mizigo zinakosa hewa na inabidi zikae tubutubu na kutoa vuke bila ya kupata hewa na kupelekea kuharibika kuta za nyumba.
Anaongeza kuwa ni lazima kuweko kwa utaratibu kila wakfu unatakiwa uwe na akaunti yake na kila wakfu ni lazima kutumia mapato yake.
Alifahamisha kuwa Kamisheni ya Wakfu inasimamia mfuko wa mali husika kwa kuhakikisha wanufaika wanapata haki zao kwa mwaka iwe familia au taasisi kama misikiti pamoja na kuangalia kwa kiasi kitakachoweza kufanyiwa matengenezo na kuhakikisha hesabu zinakwenda vizuri bila ya kudhulumu.
Vile vile, katika kusimamia ni muhimu kutunza kumbukumbu za Wakfu husika alisema msimamizi wa mali za Wakfu iwe kumbukumbu za wapangaji, matengengezo, wanufaika pamoja na wakfu wenyewe ( Nyaraka ) na hii itarahisisha kuweza kujuwa malipo ya watu wangapi yamefanyika au laa.
Mkuu huyo alisema matengenezo ya nyumba umeshafanya mara ya ngapi na je nyumba hii inaleta tija au haileti tija?
Alitoa wito wa Kuweka Wakfu kwa waumini wa dini ya kiislamu ambapo alisema ni jambo zuri kwa maisha ya duniani na akhera.
BAADHI ya majengo yanayosimamiwa na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar.