WARSHAWA, POLAND

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeitaka Poland kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka Iraq na Afghanistan ambao wamekwama kwenye mpaka wa nchi hiyo na Belarus kwa zaidi ya wiki mbili.

UNHCR ilionyesha wasiwasi juu ya ripoti za kutisha za baadhi  ya watu waliokwama mpakani, na kwamba wakimbizi hao wanahitaji matibabu ya dharura na ulinzi wa kimataifa.

Maelfu ya wahamiaji, wengi kutoka Mashariki ya kati, wamevuka mpaka wa Belarus na wanaelekea katika mataifa ya mashariki mwa Umoja wa Ulaya yakiwemo Latvia, Lithuania na Poland katika miezi ya hivi karibuni.

Umoja wa Ulaya unaamini kuwa ujio wa wakimbizi hao umefanywa kwa makusudi na Belarus, ikiwa kama njia ya kulipiza kisasi baada ya utawala wa Alexander Lukashenko kuwekewa vikwazo na EU.