ZASPOTI
MWENYEKITI msaidizi wa timu ya Al-Azzar ya Mtambwe, Khalifa Said Hamad, amesema, hawatamuonea muhali kiongozi yoyote atakayekuwa hana ushirikiano katika utendaji wa majukumu yao.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kufuatia utendaji mdogo uliopo kwa baadhi ya viongozi wa timu hiyo.

Alisema kumekuwa na baadhi ya viongozi kujiweka nyuma wakati timu inapokaa vikao na kugawana majukumu ya utendaji ya kazi hasa ya kifedha.
“Hii hali inaturejesha nyuma maana viongozi wanakuwa wengi, lakini, katika michango hawaonekani, hivyo tuko tayari kumruhusu kiongozi kuondoka kama atashindwa kutoa ushirikiano”, alisema.

Aidha, alisema, wanatarajia kufanya usajili wa wachezaji sita ikiwemo kipa mmoja washambuliaji wawili na viungo watatu.
“Kati hao tutakaowasajili, wanne tutawachukuwa katika mashindano yetu ya Yamle Yamle Nondo Cup tunayotarajia kucheza katika hatua ya 36 bora”, alisema.

Akizungumzia juu ya kushiriki mashindano hayo, alisema, wamejipanga kushinda hatua hadi hatua na kufikia kuchukuwa ubingwa msimu huu.
Hivyo, aliwataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza ili kuwapa nguvu wachezaji wao.