KAMPALA, UGANDA
KIKOSI cha usalama cha polisi na jeshi kimewaonya wakaazi wanaotaka kutembelea eneo la Karamoja kuacha kutumia pikipiki kufikia eneo hilo.
Onyo hilo limetolewa na Msemaji wa Polisi wa Mkoa wa Karamoja Michael Longole, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kuendesha pikipiki kupitia njia za ndani kama vile Moroto, Kotido, Moroto, Nakapiripirit, Moroto Nabulatuk inapaswa kufungwa kipindi hichi wakati zoezi la kupokonya silaha linafanyika.
Wito wa Longole unafuatia mashambulio endelevu kwa watembea kwa miguu wanaopanda pikipiki haswa kwenye barabara ya Moroto-Kotido na wezi wa mifugo wenye silaha.
Wiki iliyopita, Abraham Lomongin, mwenye umri wa miaka 23 mkaazi wa Wilaya ya Napak aliuawa kwa kupigwa risasi na wapiganaji wenye silaha wakati akiwa amepanda pikipiki akielekea Wilaya ya Kotido.
Kikosi cha pamoja cha usalama cha polisi na jeshi kimekuwa kikipambana na wezi wa mifugo wenye silaha tangu Julai 17, mwaka huu wakati awamu ya pili ya zoezi la upokonyaji silaha lilipozinduliwa.
Kapteni Edrine Mawanda, msemaji wa kitengo cha tatu cha UPDF alisema tangu walipoanzisha awamu ya pili ya upokonyaji silaha, wamepata bunduki 52 kutoka kwa mikono ya wezi wa ng’ombe wa Karamojong kupitia njia zote za hiari na za nguvu.
Kapteni Mawanda ameongeza kuwa jumla ya wizi wa ng’ombe 300 walikamatwa na watafikishwa katika mahakama ya kijeshi kukabiliwa na mashitaka ya kupatikana na silaha, mauaji, na wizi kinyume cha sheria.