WIKI chache baada ya Marekani na nchi za Magharibi kutangaza kuondosha vikosi vilivyokuwa vitani kwa takriban miaka 20 nchini Afghanistan, hatimaye utawala wa nchi hiyo umepinduliwa na kuchukuliwa na wapigananji wa kundi la Taliban.

Waasi hao wamechukua zaidi ya dazeni moja ya miji mikuu ya mikoa katika wiki moja na kuuzingira mji mkubwa zaidi eneo la kaskazini, katika ngome ya asili ya upinzani dhidi ya Taliban wa Mazar-i-Sharif.

Mnamo mwaka 2001, Marekani na baadhi ya nchi wanachama wa Nato waliwafurusha watalibani kutoka Kabul baada ya mashambulio ya 9/11 yaliyotokea New York na Washington, ambayo yanaelezwa kuwa yaliratibiwa na Osama bin Laden.

Baada ya wataliban na washirika wao kundi la Al Qaeda kusukumwa nje ya mji wa Kabul, ilichukua miaka kadhaa kujipanga tena na mnamo mwaka 2004 walikuwa katika nafasi ya kuanzisha uasi dhidi ya vikosi vya magharibi na serikali mpya ya Afghanistan.

Vita nchini Afghanistan vilikuwa virefu vilivyokuwa na gharama kubwa ambapo kwa mujibu wa taarifa vita hivyo vimepoteza zaidi ya dola bilioni 978 na maelfu ya maisha ya askari na wananchi yamepotea.

Rais wa Marekani Joe Biden ametetea uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi kutoka Afghanistan, akisema uamuzi huo ni wenye tija kwa maslahi ya nchi yake.

Biden amekiri kuwa serikali ya Afghanistan ilisambaratika haraka kuliko alivyotarajia, lakini aliilaumu serikali ya mjini Kabul kwa kushindwa kupigana na Wataliban licha ya misaada na mafunzo chungu nzima kutoka Marekani.

Biden alisema wanajeshi wa nchi yake hawawezi kuendelea kutoa maisha yao kwa niaba ya Waafghanistan wasio na nia ya kuipigania nchi yao na kuongeza kuwa yuko tayari kubebeshwa lawama kwa kumaliza uwepo wa miaka 20 wa nchi yake nchini Afghanistan, kuliko kuurefusha uwepo huo na kuurithisha kwa rais atakayefuata.

“Nashikilia msimamo wangu bila kutetereka, baada ya miaka 20 nimejifunza ukweli mchungu, kwamba hakuna wakati bora wa kuondoa vikosi vya Marekani, hiyo ndio sababu bado tuko kule, tulijua bayana hatari iliyopo”, alisema Biden.

Kumekuwa na kauli mbalimbali zinazotolewa duniani baada ya kundi la Taliban kufanikiwa kuchukua madaraka, ambapo zaidi ya mataifa 60 yalitoa kauli ya pamoja.

Marekani na nchi nyingine zikiwemo Australia, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Korea Kusini na Uingereza katika kauli yao ya pamoja zimesema walio katika nafasi na madaraka nchini Afghanistan wanalo jukumu na wanawajibika kulinda maisha ya watu na mali ili kuhakikisha amani, ulinzi na maisha ya kila siku yanarejea katika hali ya kawaida.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Urusi, Maria Zakharova ameibebesha lawama Marekani akisema, dunia inaendelea kushuhudia kwa hofu matokeo ya majaribio ya kihistoria ya Marekani.

Zakharova alisema kuwa madai ya Marekani kwamba imefanikiwa kutekeleza malengo nchini Afghanistan ambayo ni kuliangamiza kundi la Taliban ni ndoto.

Alieleza kuwa maofisa wa serikali ya Marekani wametoa madai mengi wakisema kuwa wamefikia malengo yao huko Afghanistan lakini kwa sasa wanapaswa kuulizwa kuhusu ndoto hiyo kwamba, malengo hayo ya awali yaliainishwa na nani?

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan alisema serikali yake itaendeleza kila juhudi kuisaidia Afghanistan ili kuhakikisha nchi hiyo inakuwa na utulivu na kuongeza kuwa taifa jirani la Pakistan lina jukumu la msingi katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Pakistan yenyewe kupitia kwa waziri wake wa mambo ya kigeni Shah Mahmood Qureshi imesema wakati utakapofika, itaitambua serikali ya Taliban kwa kuzingatia makubaliano ya pamoja ya kimataifa.

Lakini waziri mkuu wa Pakistan, Imran Khan alizungumzia hatua hiyo ya Taliban kuidhibiti Afghanistan akisema taifa hilo hatimaye limejifungua kutoka kwenye minyororo ya utumwa baada ya kumalizika kwa vita vya miaka 20 bila ya machafuko.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa ulimwengu kushirikiana katika kupambana na kitisho cha ugaidi nchini humo.

Guterres aliuambia mkutano wa dharura wa baraza la usalama la umoja huo kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha Afghanistan haiwi tena jukwaa ama eneo litakalotumiwa na makundi ya kigaidi kuendeleza shughuli zao.

Msemaji wa kundi la Taliban, Suhail Shaheen ametaka iundwe serikali ya kiislamu nchini Afghanistan inayoendana na mazingira itakayojumuisha na Waafghani wengine pia.

Halikadhalika msemaji huyo wa Taliban amesema, kundi hilo litawahakikishia usalama wanajeshi na askari wa vikosi vya usalama watakaokabidhi silaha zao na kujiunga na kundi hilo.

Kabla ya tangazo hilo, viongozi wa Taliban waliliambia gazeti la Times la Uingereza kuwa kundi hilo haliafiki wazo la kuundwa serikali ya mpito nchini Afghanistan.

Agosti 15 mwaka huu wapiganaji wa Taliban waliiingia mji wa Kabul na kuiteka kasri ya rais ambaye inasemekana amekimbilia nchi jirani kuombahifadhi na baadhi ya viongozi wa nagazi ya juu wa nchi hiyo.

Baada ya kuikalia ardhi ya Afghanistan kwa kipindi cha miaka 20 Marekani imeshindwa kuliangamiza kundi la Taliban ambalo sasa limeshika tena madaraka ya nchi hiyo.

Taarifa kutoka nchini Afghanistan zinaeleza kuwa katika kipindi cha miaka 20 ya uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ugaidi ulitanuka zaidi na kuongezeka kwa biashara na uzalishaji wa dawa za kulevya.