JAKARTA, INDONESIA

IDADI ya vifo vilivyotokana na virusi vya korona imezidi 100,000 nchini Indonesia.Nchi hiyo imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la idadi ya maambukizi mapya tangu mwezi Julai.

Serikali inasema idadi ya vifo ilikuwa 100,636 hadi kufikia sasa.Vifo takribani 35,000 vilitokea mwezi Julai pekee wakati kukiwepo na ongezeko kubwa la aina mpya ya virusi ya Delta inayoambukiza kwa kasi zaidi.

Maambukizi yaliyothibitishwa yaliongezeka kati ya 30,000 hadi 50,000 kwa siku.Idadi ya vifo pia ni kubwa mno, ikiwa zaidi ya vifo 1,500 kwa siku.

Serikali ya Indonesia inaongeza jitihada zake za kujenga vituo vya muda vya kujitenga vilivyo na madaktari na wauguzi kwani wagonjwa wengi wamefariki wakati wakipata nafuu nyumbani.

Serikali pia imetuma vikosi na maafisa wa polisi kuwapeleka watu walioambukizwa virusi hivyo kwenye vituo vya kujitenga.