NA MADINA ISSA
VIJANA wa makundi maalum ya Hamasa na Itifaki wamehimizwa kuendelea kujitokeza katika kushiriki shughuli za ujasiriamali pasipo kukata tamaa, ili kujijengea uwezo mzuri wa kujituma na kujiongezea kipato.
Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa UVCCM, Stella Cassian Mbawala, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na vijana hao baada ya kumalizika ziara yake aliyoifanyika kwa vijana wa wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini Unguja.
Alisema miongoni mwa sababu zilizopelekea kuwepo makundi hayo ni kuwajengea uzalendo katika kutafuta njia bora za uzalishaji, ili kuweza kujiajiri wao wenyewe kutokana na sekta ya kilimo wanachokifanya katika makundi yao.
Alisema Chama cha Mapinduzi pamoja na serikali inatambua uwepo wao kama vijana imara waliojengeka, hivyo aliwataka watumie uwezo walionao katika kubuni miradi zaidi ikiwemo ya kilimo na kuomba serikali itowe kipaumbele zinapotokea nafasi wanazoweza kuzitumikia kiajira.
Aidha, aliwahimiza umuhimu wa vijana na kuendelea kuchukuwa tahadhari juu ya kujikinga na ugonjwa wa covid 19, ambao kuendelea kuwepo kwake unaathiri maendeleo ya kiuchumi.
Nae Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja, Mohammed Ali Kawaida, alisema kamati yao ya uongozi wanaangalia namna bora ya kuweza kutafuta fedha kwa ajili kuweka miradi ya uhakika, ili kuepuka makundi hayo kutegemea misaada.
Aidha, alimpongeza Mjumbe huyo kwa kujitolea kuwasaidia vijana hao na kusema kuwa amekuwa akionesha ushujaa wa kiongozi na namna inavyotakiwa katika uongozi aliokuwa nao.
“Kuwapatia vijana msaada huu wa chakula imeonesha wazi kuwa kiongozi huyu amekuwa akijali vijana wenzake ambapo ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wenzake” alisema.