NA ASYA HASSAN

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini kichama, Talib Ali Talib, amesema ni vyema vijana kujikita zaidi kusoma historia ya nchi yao, ili kuepuka kudanganywa na baadhi ya watu wasiolitakia mema taifa hili.

Talib alisema hayo huko Amani Mkoa alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya darasa maalum la itikadi la kikosi kazi kwa vijana 65 wa CCM Mkoa wa Mjini.

Alisema hatua hiyo pia itasaidia kuthamini juhudi zilizofanywa na waasisi wa nchi yao, pamoja na kuziendeleza kwa kuleta maslahi mapana ya nchi yao.

Mwenyekiti huyo, alifahamisha kwamba nguvu kazi ya taifa inategemea vijana hivyo kuna kila sababu kujuwa historia yao pamoja na dhana nzima ya uzalendo ambayo ndio itayochangia kufanya shughuli  zao za kimaendeleo kwa mslahi mapana ya nchi.

Sambamba na hayo alifahamisha kwamba Zanzibar inahistoria tofauti na za miaka mingi, hivyo ni vyema vijana wakazisoma vizuri ili ziwasaidie kujua utu na thamani iliyowekwa na muasisi wa nchi hii.

Mbali na hayo, Mwenyekiti huyo aliwasisitiza vijana hao kuendeleza Amani, umoja, mshikamano na utulivu uliyopo hapa nchini, kwani hiyo ndio silaha madhubuti ya kufanikisha harakati mbalimbali za kimaendeleo ndani ya nchi hii.

Aidha alitumia fursa hiyo, kuwataka vijana hao kuyakamata masomo hayo na kuyafanyia kazi, ili yaweze kuwa na tija kwao na taifa kwa ujumla.

Mbunge wa Jimbo la Amani Mussa Hassan ambae ni mlezi wa vijana hao akiwasilisha madq ya uzalendo alisema bila ya muungano hatoweza kuwa na nguvu moja katika kufanya kazi hivyo aliwataka vijana hao kuulinda na kuuenzi muungano huo.

Sambamba na hayo, Mbunge huyo huyo aliwasisitiza vijana hao kuhakikisha wanalinda na kudumisha amani, umoja na mshikamano ulioachwa na waasisi wa nchi hizi mbili.

“Fikra za waasisi hao zinawafunza vijana kuwa wazalendo na nchi yao ili kufanikisha malengo ya mapinduzi na muungano wa nchi hizi mbili,”alisema.