NA HAFSA GOLO

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imeshauriwa kusomesha wavuvi wa meli za uvuvi (fisherman), ili kutumia vyema teknolojia ya dunia na kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) Sheha Ahmeid Mohamed, alitoa ushauri huo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Malindi Mjini Unguja.

Alisema iwapo serikali itafanya juhudi  za makusudi kuwasomesha vijana hao itasaidia  kutimiza azma ya ununuzi wa meli mpya za kisasa  na hatimae  kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar .

Sheha alisema, uendeshaji wa meli za kisasa kunahitajika wataalamu wenye elimu ya kuitambua teknolojia ambazo zimo ndani ya meli hizo.

“Imefika wakati lazima serikali iangalie kwa kina suala hilo ili kuondokana na changamoto zilizotokeza awali katika Meli ya MV Mapinduzi II, na kusababisha kuleta matatizo ya kiufundi ndani ya maeli hiyo ambayo ulitumia gharama kubwa ya fedha  ”.alisema.

Alifahamisha kwamba kitendo cha kusomesha vijana wazalendo kitawezesha kupiga hatua za maendeleo katika mageuzi ya kiuchumi sambamba na kuondokana na utendaji wa mazoea.

Akitilia mkazo alisema bila ya wataalamu hakuna kitachofanyika hasa katika mikakati iliyowekwa na serikali katika kutumia fursa za uchumi wa baharini.