NA TATU MAKAME

VIJANA nchini wametakiwa kuchangamkia fursa zitokanazo za uchumi wa buluu na uvuvi ili kujikwamua na hali ya utegemezi.

Mkurugenzi Uratibu na maendeleo ya uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Bakari Hamad alisema hayo ofisini kwake Maisara wakati akizungumza na gazeti hili  katika ofisi za wizara hiyo maisara Mjini Zanzibar.

Katika mkutano huo, wadau walijadili mapitio ya rasimu ya sera ya uchumi wa buluu mpango mkakati wa utekelezaji wa sera ya mwaka 2020 ambayo inayofanyiwa marekebisho kupitia sera mpya ya  mwaka 2021.

Alisema sera hiyo itaangalia zaidi makundi maalum yakiwemo ya vijana, watu wenye ulemavu na makundi mengine ikiwa ni kutekeleza mpango endelevu wa uchumi wa buluu nchini hivyo ni vyema kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema kuwa sera ambayo inafanyiwa marekebisho haikutoa vipaumbele kwa watu hao hivyo wizara imeona ipo haja ya kufanya marekebisho sera mpya yam waka 2021 ili kila kundi lifaidike na fursa za uchumi.

Mapema akiwasilisha mada kuhusu mpango mkakati wa sera ya uchumi wa buluu, Ali Haji Ramadhan, kutoka wizara hiyo alisema mchango wa kila mwananchi unahitajika katika kutekeleza sera hiyo.

“Tumeangalia vipaumbele kwa kundi la vijana na watu wenye ulemavu ili kila mwananchi aweze kunufaika na sera hii,” alisema.

Sambamba na hayo alisema katika kuipitia sera hiyo wataangalia masuala ya bahari juu ya ushirikishwaji wa wananchi kwenye uchumi huo kuwapa nafasi ya kutekeleza sera hiyo.

“Tunapozungumzia uchumi wa buluu kuna uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja, kila mtu ananafasi yake juu ya uchumi huo,” alisema.

Mapema wakitoa mapendekezo yao juu ya sera iliyopo wadau kutoka taasisi mbalimbali waliitaka Wizara kuweka mkakati wa mawasiliano kwenye utekelezaji wa resa mpya ili kila mtu atowe mapendekezo yake.

Salim Ali Bakari kutoka Idara ya Mazingira na Salma Hamad Suleiman kutoka kampuni ya uvuvi Zanzibar (ZAFICO) alisema ipo haja ya kupatiwa elimu ya uvuvi kwa watumishi na wananchi ili kufikisha elimu hiyo kwa jamii inayowazunguuka.