NA KHAMISUU ABDALLAH

VIJANA wametakiwa kuwa wazalendo katika kutumia muda wao kwa kujiamini katika kuhakikisha inatumia fursa zilizomo katika nchi yao katika kujiajiri na kuweza kuleta maendeleo.

Mwakilishi wa Jimbo la Pangawe, Ali Suleiman Ameir ‘Mrembo’, alitoa kauli hiyo wakati akifungua kongamano la wanawake na vijana, liloandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana (BIWO) lilofanyika katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo.

Alisema serikali imekuwa ikihabarisha fursa zinazopatikana katika uchumi wa bluu kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo ya mafuta na gesi, uvuvi pamoja na utalii hivyo ni jukumu la vijana kutumia fursa hizo.

Aidha, alisema ikiwa vijana watatumia fursa hizo basi yale maendeleo yanayotafutwa katika maeneo hayo basi yataweza kupatikana kwa wakati sahihi.

“Kwa sasa mchakato wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi unaendelea ni wajibu wenu kujifunza, ili jambo hili likiwa limekaa tayari basi nyinyi muwe tayari kuchangamkia fursa hizo,” alisema.