NA ABOUD MAHMOUD

JUMLA vikundi 23 kutoka mataifa mbali mbali ya Afrika vimepata nafasi ya kushiriki tamasha la Sauti za Busara linalotarajiwa kurindima Febuari 11 hadi 13 mwakani katika viwanja vya Ngome Kongwe.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisi za Busara Maisara mjini Unguja, Meneja wa tamasha hilo Journey Ramadhan alisema taasisi yake ilipokea maombi 350 kutoka katika vikundi mbali mbali duniani kuanzia mwezi Mei hadi Julai 31 mwaka huu.

Alisema mara baada ya kufanya  ukaguzi vikundi vilivyoomba taasisi hiyo ilichagua vikundi 23, ambayo waliona vitafaa kutoa burudani katika tamasha hilo ambalo mwakani litatimiza miaka 19 tangu kuanzishwa kwake.

“Tayari tumechagua vikundi ambavyo vitashiriki kutoa burudani mwakani katika tamasha letu la 19, ambapo  vikundi vingi viliomba kushiriki, lakini hatuwezi kuvichukua vyote imetulazimu tuchague na tumepata 23 ambavyo vitapanda kwenye jukwaa la busara,”alisema.

Journey alivitaja vikundi vilivyofanikiwa kuchaguliwa kushiriki katika tamasha la mwakani ni  pamoja na wenyeji Zanzibar vikundi 3, Tanzania Bara 2, Uganda 1, Afrika Kusini 5, Zimbabwe 2, Zambia 1, Ivory Coast 1, Moroko 1, Msumbiji 1, Island ya Kaskazini 1, Reunion 1, Kongo 1 na Tunisia 1.

Aidha meneja huyo alisema taasisi ya busara imepanga kuwaalika wasanii maarufu ambao wataweza kuja kutoa burudani katika tamasha hilo.