NA HAFSA GOLO
TUME ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kuwapatia mafunzo ya maadili viongozi wa umma, ili yawasaidie kutambua miiko na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Asaa Ahmada Rashid, wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Vuga mjini Unguja, alisema mafunzo hayo yatakwenda sambamba na mikutano ngazi ya shehia vyuo vikuu na skuli ambapo utekelezaji wake utakuwa miezi mitatu kuazia Septemba hadi Novemba mwaka huu.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia viongozi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, ili wasifanye makosa.
Aidha alisema mafunzo hayo pia yatawasaidia kufanya kazi kwa kuzingatia uwazi,kufuata sheria,kanuni na miongozo ya kazi katika uwajibikaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Ni jambo la wajibu kwa viongozi kufuata na kuzingatia sheria kanuni na miongozo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi”,alisema.
Mwenyekiti huyo alisema lengo jengine la utekelezaji wa hatua hiyo ni kuimarisha utawala bora wenye kuzingatia matakwa ya kisheria,haki na wajibu katika utoaji wa huduma na kuleta ufanisi wa kiutendaji.
Alifahamisha kwamba miongoni mwa mambo mengine ya msingi watakayoelezwa viongozi hao ni pamoja na namna bora ya kukabiliana na migongano wa maslahi binafsi katika utekelezaji wa kazi, ili haki na wajibu ichukue nafasi yake.
Kuhusu mikutano ya wananchi alisema, tume hiyo itawaeleza na kuwafundisha umuhimu wa maadili na namna ya utoaji wa taarifa zinazowahusu viongozi.
Alisema mikutano hiyo itasaidia kuwajengea uwezo wananchi wa kufahamu makosa husika yanapostahiki kulalamikiwa.
“Tumekuwa tukipokea baadhi ya malalamiko ambayo hayastahiki kuletwa hapa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria badala yake yake yanatakiwa kufikishwa kwenye vyombo vyengine vya kisheria, hivyo mikutano hii itasaidia kuwaelimisha wananchi kutambua malalamiko na viongozi wanaostahiki kulalamikio katika Tume hiyo”,alisema.