NA MWANAHAWA HARUNA SCCM

WALIOKOSA vyandarua wametakiwa kuripoti kwa Masheha wao ili kupatiwa Vyandaruwa kwa lengo la kuhakikisha Serikali inatokomeza malaria Zanzibar.

Hayo yameelezwa na Ofisa Uhamasishaji na msimamizi wa Vyandaruwa kitengo cha kumaliza malaria Zanzibar, Mwinyi Khamis, huko Ofisini kwake Mwanakwerekwe Mjini Unguja, wakati akielezea uendeshaji zoezi la utowaji wa vyandarua katika baadhi ya Wilaya za Unguja na Pemba.

Alisema kuwa katika zoezi la utowaji wa Vyandarua unaoendelea hapa nchini ambalo katika baadhi ya Wilaya na shehiya limemalizika kwa mujibu wa uhakiki waliofanya kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kutokuhakikiwa na kupelekea kukosa Vyandarua.

Alifafanua kuwa wakati wa utowaji vyandarua kuna badhi yao wanakuja na wanarudishwa kwa kuwa hawakuhakikiwa kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo kusahauliwa kwa baadhi ya kaya au zarura ambayo iliwafanya wasisajiliwe hakukuwa na taarifa zao.

Aidha, alisema wanatarajia kutoa Vyandaruwa kwa shehiya 335 na hadi hivi sasa washatoa katika shehiya 311, bado shehiya 24 tu ambazo wanatarajia kumaliza mwezi wa Agosti na walitarajia kutoa jumla ya Vyandarua 747,000.

Hivyo amewataka wananchi ambao hawakupata Vyandaruwa baada ya zoezi la mwazo kumalizika warudi kwa masheha wao wasajiliwe na wao waweze kupatiwa.

“Waliokosa Vyandarua wanatakiwa warudi kwa masheha wao wakafanyiwe usaili na waweze kupatiwa vyandarua kwani tunavyandaruwa vya kutosha lengo ni kuhakikisha kuwa wale wote walengwa anahakikishwa kuwa anapata chandaruwa cha kujikinga na malaria”,alisema Mwinyi.