NA KHAMISUU ABDALLAH

 SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema, lengo la kuifanyia marekebisho Sheria namba 9 ya dawa za kulevya ya mwaka 2019 ni kuipa nguvu taasisi inayoratibu na kuendesha vita dhidi ya biashara hiyo.

Sheria hiyo imelenga pia kuibadilisha taasisi hiyo kuwa na mamlaka ya kuchunguza, kukamata na kufungua mashauri mahakamani ili kupambana kikamilifu na watu wanaojihusisha na biashara ya dawa hizo nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema hayo jana wakati akifungua mkutano wa kujadili marekebisho ya sheria dawa za kulevya ulioshirikisha wadau kutoka taasisi za serikali na binafsi uliofanyika katika ukumbi wa kitengo cha uzazi shirikishi Zanzibar,  Kidongochekundu.

Alisema marekebisho yanayotarajiwa kufanyika yamelenga kuondoa mapungufu na changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika utekelezaji wa sheria inayotumika sasa.

Dk. Mkuya alisema kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2012, ulibaini kuwa vijana 10,000 wameingia katika athari ya utumiaji wa dawa za kulevya, jambo ambalo halikubali kwani vijana wengi wanapoteza muelekeo wa maisha yao na taifa kupoteza nguvu kazi inayotegemewa katika kujenga nchi yao.

Akizungumzia lengo la kuwaita wadau hao alisema wao ni watu muhimu katika kutoa michango yao katika maandalizi yote ya sheria hiyo kwani lazima sheria hiyo ipate wadau mbali mbali kabla ya kuipeleka katika Baraza la Wawakilishi na kusomwa kwa mara ya kwanza kabla ya kuwa sheria kamili.

Awali Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Omar Dadi Shajak, alisema kabla ya miaka 1980 dawa maarufu za kulevya Zanzibar zilikuwa ni bangi na kasumba lakini kuimarika kwa biashara huria na utandawazi kumeibuka aina mpya ya dawa za kulevya kama heroine, kokeni, mandras na amfetamin.

“Sambamba na hayo sheria hiyo baadae ilifutwa kwa sheria namba 16 ya udhibiti wa dawa za kulevya ya mwaka 2003 ambayo pia ilifutwa mwaka 2009,” alieleza Dk. Shajak.

Alisema sheria ambayo inafanya kazi hivi sasa namba 9 ya udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya ya mwaka 2009, imeshafanyiwa marekebisho kupitia Sheria namba 12 ya mwaka 2011, sheria namba 5 ya mwaka 2016 na Sheria ya mwaka 2019.

“Pamoja na marekebisho hayo, sheria hiyo haijaipa uwezo wa kisheria wa kukamata, kupeleleza pamoja na kufungua mashauri mahakamani taasisi iliyopewa dhamana ya kuratibu masuala hayo jambo ambalo ni changamoto,” alieleza Dk. Shajak.

Alibainisha kuwa katika kukabiliana na mapambano hayo serikali imeamua kuifanyia marekebisho taasisi ya kupambana na dawa za kulevya kuwa mamlaka kamili yenye uwezo wa kuchunguza, kukamata na kupeleleza kesi za dawa hizo nchini.

Akiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, Mkurugenzi Uchunguzi na Mwanasheria wa Tume ya uratibu wa Dawa za Kulevya, Juma Zidi Kheir, alisema sheria hiyo itaondoa dhamana kwa watu watakaopatikana na dawa za kulevya hadi mashauri yao yatakapokamilika.

Alisema lengo la sheria inayopendekezwa inatokana na nia ya serikali ya kutekeleza kwa vitendo udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambapo itataifisha mali na vitu vinayotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Alibainisha kuwa sheria hiyo imezingatia matakwa ya mikataba ya kimataifa ya mwaka 1961, 1972, 1988 pamoja na marekebisho yao kwa kuanzisha makosa kama ilivyoelezwa katika mikataba hiyo.

Akizungumzia sababu za kuwepo kwa sheria hiyo inayopendekezwa alisema kutasaidia kupunguza kazi ya makosa yanayohusiana na dawa za kulevya na kutekelezwa ipasavyo sheria hiyo ikiwemo kutaifishwa kwa mali zinazotokana na dawa hizo.